Ijumaa, 24 Aprili 2015

TOGO KUMCHAGUA RAIS MPYA JUMAMOSI.

Wapiga kura nchini Togo watamiminika vituoni kesho Jumamosi kumchagua rais mpya kwa muhula mingine wa miaka mitano. Rais wa sasa Faure Gnassingbe, ndiye anatarajiwa kuibuka mshindi katika ya wagombea watano. Amekuwa uongozi tangu mwaka 2005 baada ya kumrithi babake ambaye aliitawala Togo kwa miaka 38. Uchaguzi huo unafanyika licha ya kuwepo malalamiko kutoka kwa upinzani na mashirika ya umma kuhusu kutokuwepo mabadiliko ambayo yatapunguza mihula ya rais. Upinzani ulilalamikia uchaguzi wa mwaka 2005 na 2010, ukikishutumu chama kinachoongoza kwa wizi wa kura. Rais wa Ghana na mkuu wa Ecowas Dramani Mahama ambaye aliizuru Togo mara mbili zaidi ya siku 30 zilizopita ametaka kuwepo uchaguzi wa amani. Gnassingbe Eyadema, babake rais wa sasa aliaga dunia mwaka 2005 baada ya miaka 38 uongozini, baada ya kuingia madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1967.

BBC.

WASHUKIWA WA UGAIDI WAKAMATWA ITALIA.

Polisi nchini Italia wanasema kuwa wamewakamata watu 18 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Islamic State kutoka nchini Afghanistan na Pakistan katika oparesheni kubwa ya kupambana na ugaidi. Wanasema kuwa wawili kati ya washukiwa hao wanaaminiwa kuwa walinzi wa aliyekuwa kiongozi wa al-Qaeda Osama Bin Laden na wengine wanashukiwa kuhusika kwenye mashambulizi nchini Pakistan likiwemo shambulizi lililotokea kwenye soko la Peshawar. Oparesheni hiyo ilikuwa imeendeshwa kwenye kisiwa cha Italia cha Sardina . Polisi walisema kuwa kundi linalofanyiwa uchunguzi lilikuwa limewapangia wanachama wake kuingia nchini Italia wakiwa na vyeti vya kufanya kazi au kama watafuta hifadhi.

BBC.

Alhamisi, 9 Aprili 2015

IRAN YATAKA VITA DHIDI YA HOUTHI KUKOMA.

Rais wa Iran Hassan Rouhani, ametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulio dhidi ya wapiganaji wa Kihouthi nchini Yemen, akiyataja kama makosa makubwa. Iran pia imepinga madai ya Saudi Arabia kuwa utawala wa Tehran unawapa wapiganaji hao wa Kihouthi ambao ni wa shia mafunzo ya Kijeshi. Balozi wa Saudi Arabi mjini Tehran, alishutishwa kufika mbele ya wizara ya mambo ya nje ya Iran, kupokea rasmi malalamishi ya Iran. Nchini Yemen, Ndege za kivita za muungano unaongozwa na Saudi Arabia, zimefanya mashambulio zaidi ya anga dhidi ya wapiganaji wa Houthi katika maeneo ya Kaskazini, Kusini na kati kati mwa Yemen. Wapiganaji hao wa Houthi ambao wanapinga utawala wa rais Abd Rabbu Mansour Hadi, wamechukua uthibiti wa maeneo kadhaa nchini humo katika miezi ya hivi karibuni. Akiongea mjini Tehran, rais Rouhani alitaja mashambulio hayo kama makosa makubwa. Awali waziri wa mambo ya nje wa Marekani John kerry alionya Iran dhidi ya kuwaunga mkono wapiganaji hao wa Houthi. Kerry aliyasema hayo baada ya Iran kutuma manuwari mbili za kijeshi katika eneo la Guba la Aden.

BBC.

PALESTINA WAUNGANA NA SYRIA KUWATIMUA IS.

Raia wa Palestina wanasema kuwa wamekubali kushirikiana na serikali ya Syria ili kujaribu kuwafurusha wapiganaji wa IS nje ya kambi moja ya wakimbizi viungani mwa Damascus. Tangazo hilo hilo lilifanywa na afisa mmoja wa serikali ya Palestina huko West Bank. Wapiganaji wa IS walitekeleza shambulizi katika kambi hiyo wiki iliopita na kuweza kuiyumbisha kanbi hiyo licha ya pingamizi kutoka kwa jeshi la Palestina. Takriban wakimbizi elfu kumi na nane wanaishi katika kambi hiyo ambayo inakabiliwa upungufu mkubwa wa vitu muhimu.

BBC.

JAJI NA WAKILI WAPIGWA RISASI ITALY.

Jaji mmoja na wakili ni miongoni mwa watu waliouawa baada ya mshukiwa mmoja kuwafyatulia risasi ndani ya mahakama moja mjini Milan nchini Italia. Maafisa wa idara ya mahakama wanasema kuwa mshukiwa aliyefyatua risasi ni mtu mmoja aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kutangazwa kufilisika. Mshukiwa huyo aliwapiga risasi watu wawili ndani ya mahakama kabla ya kumshambulia jaji ambaye angelisikiliza kesi yake ndani ya ofisi yake. Mtu wa nne anaaminika kufariki kutokana na mshtuko wa moyo. Mshukiwa huyo alikamatwa kaskazini mwa Milan akitoroka kwa pikipiki. Haijulikani jinsi mshukiwa huyo alivyoweza kuingia ndani ya mahakama hiyo huku akiwa na bunduki, kwa kuwa wageni wote hupitia vifaa vya kuwakagua ikiwa wana silaha.

BBC.

MUME 1 KATI YA 10 HUPIGWA NA MKEWE KENYA.

Mmoja kati ya wanaume 10 wa Kenya amepigwa na mkewe ama mpenziwe kulingana na utafiti wa kiafya. Wanaume walio kati ya umri wa miaka 20 hadi 24 ambao ni asilimia 11.7 wamevumilia unyanyasaji huo na wamekuwa wakifuatiwa kwa karibu na wale walio na kati ya umri wa miaka 40 na 49 wakiwa asilimia 9.8. Wale walio kati ya miaka 30 na 39 waliripoti visa vichache huku asilimia 7.1 wakisema kuwa walinyanyaswa kulingana na utafiti huo wa mwaka 2014. Wanaume waliopewa talaka ama hata kutengana na wake zao waliriporti visa vya juu vya unyanyasaji. Walifuatiwa na wanaume ambao wameoa zaidi ya mara moja. Ni asilimia 7.1 ya wanaume ambao wanaishi na wake zao ambao wameripoti visa vya kupigwa. Wale ambao wameoa mara moja walikuwa na visa vichache ikilinganishwa na wale ambao wameolewa mara mbili ama hata zaidi. Wanaume ambao hawakukamilisha elimu ya msingi waliripoti visa vingi vya unyanyasaji wakifuatiwa na wale ambao wamekamilisha masomo ya msingi na yale ya shule za upili..

BBC.

Alhamisi, 2 Aprili 2015

KESSY AGOMEA PESA YA MBOGA.

KATIKA mahojiano baina ya Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na viongozi, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa akituhumiwa kukiuka maadili katika sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow alitoa kauli moja ambayo iliwafurahisha wengi. Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini, alijitetea kwamba matumizi ya Sh10 milioni alizochukua kutoka kwenye akaunti yake baada ya kuingiziwa na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira alisema fedha zilikuwa ni kwa ajili ya kununua mboga. Sasa iko hivi; unamkumbuka yule beki wa Simba aliyesajili kutoka Mtibwa Sugar anayekimbiza sana upande wa kulia? Anavaa jezi namba nne. Jamaa naye kagoma Simba anadai hela ya mboga na hayuko kwenye timu hiyo iliyokwenda Shinyanga kucheza na Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwa alichodai kuwa mpaka wammalizie fedha yake ya usajili iliyobaki na nyumba ya kuishi. Kessy alisajiliwa katika usajili wa dirisha dogo kwa makubaliano ya mkataba wa miaka miwili na dau la Sh 35 milioni na walimpa Sh 20 milioni huku ikibaki Sh 15 milioni alizoahidiwa kulipwa Januari mwaka huu. Simba iliondoka jana Jumatano kuelekea Shinyanga huku Kessy akiwa kwao Morogoro na ameliambia Mwanaspoti kuwa hatarudi Simba hadi viongozi wammalizie fedha ya usajili na nyumba ya kuishi kama mkataba unavyotaka. “Sijaenda na timu, nilirudi kwetu Morogoro tangu Jumapili, unajua haya ni maisha, inauma sana,’’ alisema.

GAZETI MWANASPOTI.

Jumatano, 1 Aprili 2015

UKEKETAJI:DESTURI HARAMU INAYOENDELEA.

Wembe mmoja hutumiwa kwa wote.

Mkeketaji huyu katika kanda ya bonde la ufa nchini Kenya ameshawakeketa wasichana wanne. Wembe alioutumia ni mmoja tu. Tendo hilo la kikatili katika desturi za kipokot linadhihirika wakati ambapo wasichana wanageuka kuwa wanawake. Ukeketaji unakatazwa katika nchi nyingi, ikiwemo Kenya. Hata hivyo, unaendelea - na zaidi katika maeneo ya wafugaji, mbali na miji.

DW.DE

MTU MWENYE UMRI MKUBWA DUNIANI AFARIKI.

Misao Okawa alifariki katika kituo cha uangalizi mjini Osaka,mji ambao alizaliwa mwaka wa 1898. Okawa amewaacha vitukuu sita na wajukuu wanne . Kufuatia kifo chake kuna madai kwamba kumesalia watu wanne pekee wanaodaiwa kuwa hai ambao walizaliwa karne ya kumi na tisa. Wote ni Wanaume huku mwanamume wa mwisho akifariki mwaka 2013.

BBC.

IS YADHIBITI KAMBI YA WAKIMBIZI SYRIA.

IS yadhibiti kambi ya wakimbizi Syria Wapiganaji wa kundi la Islamic State nchini Syria wameingia na kuchukua udhibiti wa kambi kubwa ya wakimbizi wa Palestina ya Yarmouk kandokando ya mji mkuu wa Damascus. Kambi hiyo ambayo ni nyumbani kwa watu elfu kumi na nane imekuwa ikipatikana katika mashambulizi ya udhibiti wa makaazi ya Damscus kati ya majeshi ya serikali na makundi ya waasi ambayo pia yanaipinga IS. Kuna ripoti kutoka ndani ya kambi hiyo kwamba mapigano yanaendelea kati ya wapiganaji wa IS na makundi hasimu. Maafisa wa umoja wa mataifa wameonya mwezi uliopita kwamba wakaazi wa kambi hiyo wanakabiliwa na hali ngumu huku wakikosa umeme,chakula cha kutosha pamoja na dawa.

BBC.

BUHARI AAPA KULITOKOMEZA BOKO HARAM.

Buhari aapa kulitokomeza Boko Haram Mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Nigeria Muhammadu Buhari ameelezea mashambulizi yanayotekelezwa na kundi la wapiganaji wa Boko Haram kama tatizo kuu linalokabili taifa hilo. Katika hotuba aliyotoa katika runinga za Nigeria,kiongozi huyo wa kijeshi zamani amesema kuwa serikali yake itafanya kila juhudi kuangamiza ugaidi. Vilevile amesema kuwa atakabiliana na jinamizi la ufisadi. Bwana Buhari ambaye anachukua wadhfa wa urais kuanzia mwezi ujao,alimsifu mpinzani wake na rais anayeondoka Goodluck Jonathan. Alimtaja kuwa kiongozi anayehitaji heshima.

WAZAZI WANAPASWA KUDHIBITI UNENE WA WATOTO.

Sheria madhubuti zinapaswa kutungwa ilikuzima matangazo ya kufana ya vyakula vyenye mafuta mengi. Wazazi wengi wanapuuza dalili za mapema kuwa watoto wao wamenenepa kupita kiasi. Madaktari wanasema kuwa wazazi wengi hawajui madhara ya afya kwa watoto walionenepa kupita kiasi. Katika utafiti huo uliowajumuisha zaidi ya familia 2,976 nchini Uingereza ni wazazi 4 pekee waliokuwa na shauku kuwa mtoto wao alikuwa amenenepa kupita kiasi. Madaktari wenye walikuwa wamewatambua watoto 369 kati yao waliokuwa na kiwango cha juu cha mafuta mwilini. Takwimu hizo zinaonesha kuwa watoto walionenepa kupita kiasi sasa wamekuwa kawaida tu majumbani. Watafiti hao wanaonya kuwa hili ni janga kwa afya ya jamii. Asilimia 31% ya wazazi hawajui kutambua dalili za mtoto aliyenenepa kupita kiasi Aidha utafiti huo ulielezea kuwa takriban mtoto mmoja kati ya watano ambao wanaumri wa miaka 6 tayari wanauzito unaozidi kadri kwa asilimia 14%. Kundi hilo la watafiti kutoka taasisi ya usafi ya Uingereza ''London School of Hygiene and Tropical Medicine'' lilizitembela familia 3,000 na kuwahoji iwapo watoto wao walikuwa ni wanene kupita kiasi wastani ama webamba? majibu yao yaliwaduwaza. Takriban thuluthi moja 31% ya wazazi walidunisha uzani wa watoto wao. Proffesa Russell Viner, wa chuo cha Afya ya Watoto aliiambia BBC kuwa wazazi wa kisasa wanamajukumu wengi na hivyo watoto wao hutunzwa na vijakazi asilimia kubwa ya muda ambao wazazi wako makazini mwao. Sheria madhubuti zinapaswa kutungwa ilikuzima matangazo ya kufana ya vyakula vyenye mafuta mengi. ''Hili ni janga ambalo linatokota ,madhara yake yataonekana siku za usoni katika njia ya maradhi mengi tu yanayohusiani na unene'' alisema Professa Viner. Kwa mujibu wa Dakta Dame Sally Davies, ''Afya ya watoto kwa sasa imehujumiwa na dhana kuwa japo mtu ni mnene jamii haitambagua kwani watu wengi duniani ni wanene'' "Nafikiri kwamba itatubidi tuwaelimishe wazazi kuhusiana na maswala ya afya ya watoto wao na pia kuwaeleza kuwa wanapaswa kufuatilia kwa karibu unene au sio wa watoto wao'' Anapendekeza kuwa sheria madhubuti zinapaswa kutungwa ilikuzima matangazo ya kufana ya vyakula vyenye mafuta mengi.

BBC.