Alhamisi, 9 Aprili 2015

MUME 1 KATI YA 10 HUPIGWA NA MKEWE KENYA.

Mmoja kati ya wanaume 10 wa Kenya amepigwa na mkewe ama mpenziwe kulingana na utafiti wa kiafya. Wanaume walio kati ya umri wa miaka 20 hadi 24 ambao ni asilimia 11.7 wamevumilia unyanyasaji huo na wamekuwa wakifuatiwa kwa karibu na wale walio na kati ya umri wa miaka 40 na 49 wakiwa asilimia 9.8. Wale walio kati ya miaka 30 na 39 waliripoti visa vichache huku asilimia 7.1 wakisema kuwa walinyanyaswa kulingana na utafiti huo wa mwaka 2014. Wanaume waliopewa talaka ama hata kutengana na wake zao waliriporti visa vya juu vya unyanyasaji. Walifuatiwa na wanaume ambao wameoa zaidi ya mara moja. Ni asilimia 7.1 ya wanaume ambao wanaishi na wake zao ambao wameripoti visa vya kupigwa. Wale ambao wameoa mara moja walikuwa na visa vichache ikilinganishwa na wale ambao wameolewa mara mbili ama hata zaidi. Wanaume ambao hawakukamilisha elimu ya msingi waliripoti visa vingi vya unyanyasaji wakifuatiwa na wale ambao wamekamilisha masomo ya msingi na yale ya shule za upili..

BBC.

Alhamisi, 2 Aprili 2015

KESSY AGOMEA PESA YA MBOGA.

KATIKA mahojiano baina ya Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na viongozi, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa akituhumiwa kukiuka maadili katika sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow alitoa kauli moja ambayo iliwafurahisha wengi. Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini, alijitetea kwamba matumizi ya Sh10 milioni alizochukua kutoka kwenye akaunti yake baada ya kuingiziwa na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira alisema fedha zilikuwa ni kwa ajili ya kununua mboga. Sasa iko hivi; unamkumbuka yule beki wa Simba aliyesajili kutoka Mtibwa Sugar anayekimbiza sana upande wa kulia? Anavaa jezi namba nne. Jamaa naye kagoma Simba anadai hela ya mboga na hayuko kwenye timu hiyo iliyokwenda Shinyanga kucheza na Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwa alichodai kuwa mpaka wammalizie fedha yake ya usajili iliyobaki na nyumba ya kuishi. Kessy alisajiliwa katika usajili wa dirisha dogo kwa makubaliano ya mkataba wa miaka miwili na dau la Sh 35 milioni na walimpa Sh 20 milioni huku ikibaki Sh 15 milioni alizoahidiwa kulipwa Januari mwaka huu. Simba iliondoka jana Jumatano kuelekea Shinyanga huku Kessy akiwa kwao Morogoro na ameliambia Mwanaspoti kuwa hatarudi Simba hadi viongozi wammalizie fedha ya usajili na nyumba ya kuishi kama mkataba unavyotaka. “Sijaenda na timu, nilirudi kwetu Morogoro tangu Jumapili, unajua haya ni maisha, inauma sana,’’ alisema.

GAZETI MWANASPOTI.

Jumatano, 1 Aprili 2015

UKEKETAJI:DESTURI HARAMU INAYOENDELEA.

Wembe mmoja hutumiwa kwa wote.

Mkeketaji huyu katika kanda ya bonde la ufa nchini Kenya ameshawakeketa wasichana wanne. Wembe alioutumia ni mmoja tu. Tendo hilo la kikatili katika desturi za kipokot linadhihirika wakati ambapo wasichana wanageuka kuwa wanawake. Ukeketaji unakatazwa katika nchi nyingi, ikiwemo Kenya. Hata hivyo, unaendelea - na zaidi katika maeneo ya wafugaji, mbali na miji.

DW.DE

MTU MWENYE UMRI MKUBWA DUNIANI AFARIKI.

Misao Okawa alifariki katika kituo cha uangalizi mjini Osaka,mji ambao alizaliwa mwaka wa 1898. Okawa amewaacha vitukuu sita na wajukuu wanne . Kufuatia kifo chake kuna madai kwamba kumesalia watu wanne pekee wanaodaiwa kuwa hai ambao walizaliwa karne ya kumi na tisa. Wote ni Wanaume huku mwanamume wa mwisho akifariki mwaka 2013.

BBC.

IS YADHIBITI KAMBI YA WAKIMBIZI SYRIA.

IS yadhibiti kambi ya wakimbizi Syria Wapiganaji wa kundi la Islamic State nchini Syria wameingia na kuchukua udhibiti wa kambi kubwa ya wakimbizi wa Palestina ya Yarmouk kandokando ya mji mkuu wa Damascus. Kambi hiyo ambayo ni nyumbani kwa watu elfu kumi na nane imekuwa ikipatikana katika mashambulizi ya udhibiti wa makaazi ya Damscus kati ya majeshi ya serikali na makundi ya waasi ambayo pia yanaipinga IS. Kuna ripoti kutoka ndani ya kambi hiyo kwamba mapigano yanaendelea kati ya wapiganaji wa IS na makundi hasimu. Maafisa wa umoja wa mataifa wameonya mwezi uliopita kwamba wakaazi wa kambi hiyo wanakabiliwa na hali ngumu huku wakikosa umeme,chakula cha kutosha pamoja na dawa.

BBC.

BUHARI AAPA KULITOKOMEZA BOKO HARAM.

Buhari aapa kulitokomeza Boko Haram Mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Nigeria Muhammadu Buhari ameelezea mashambulizi yanayotekelezwa na kundi la wapiganaji wa Boko Haram kama tatizo kuu linalokabili taifa hilo. Katika hotuba aliyotoa katika runinga za Nigeria,kiongozi huyo wa kijeshi zamani amesema kuwa serikali yake itafanya kila juhudi kuangamiza ugaidi. Vilevile amesema kuwa atakabiliana na jinamizi la ufisadi. Bwana Buhari ambaye anachukua wadhfa wa urais kuanzia mwezi ujao,alimsifu mpinzani wake na rais anayeondoka Goodluck Jonathan. Alimtaja kuwa kiongozi anayehitaji heshima.

WAZAZI WANAPASWA KUDHIBITI UNENE WA WATOTO.

Sheria madhubuti zinapaswa kutungwa ilikuzima matangazo ya kufana ya vyakula vyenye mafuta mengi. Wazazi wengi wanapuuza dalili za mapema kuwa watoto wao wamenenepa kupita kiasi. Madaktari wanasema kuwa wazazi wengi hawajui madhara ya afya kwa watoto walionenepa kupita kiasi. Katika utafiti huo uliowajumuisha zaidi ya familia 2,976 nchini Uingereza ni wazazi 4 pekee waliokuwa na shauku kuwa mtoto wao alikuwa amenenepa kupita kiasi. Madaktari wenye walikuwa wamewatambua watoto 369 kati yao waliokuwa na kiwango cha juu cha mafuta mwilini. Takwimu hizo zinaonesha kuwa watoto walionenepa kupita kiasi sasa wamekuwa kawaida tu majumbani. Watafiti hao wanaonya kuwa hili ni janga kwa afya ya jamii. Asilimia 31% ya wazazi hawajui kutambua dalili za mtoto aliyenenepa kupita kiasi Aidha utafiti huo ulielezea kuwa takriban mtoto mmoja kati ya watano ambao wanaumri wa miaka 6 tayari wanauzito unaozidi kadri kwa asilimia 14%. Kundi hilo la watafiti kutoka taasisi ya usafi ya Uingereza ''London School of Hygiene and Tropical Medicine'' lilizitembela familia 3,000 na kuwahoji iwapo watoto wao walikuwa ni wanene kupita kiasi wastani ama webamba? majibu yao yaliwaduwaza. Takriban thuluthi moja 31% ya wazazi walidunisha uzani wa watoto wao. Proffesa Russell Viner, wa chuo cha Afya ya Watoto aliiambia BBC kuwa wazazi wa kisasa wanamajukumu wengi na hivyo watoto wao hutunzwa na vijakazi asilimia kubwa ya muda ambao wazazi wako makazini mwao. Sheria madhubuti zinapaswa kutungwa ilikuzima matangazo ya kufana ya vyakula vyenye mafuta mengi. ''Hili ni janga ambalo linatokota ,madhara yake yataonekana siku za usoni katika njia ya maradhi mengi tu yanayohusiani na unene'' alisema Professa Viner. Kwa mujibu wa Dakta Dame Sally Davies, ''Afya ya watoto kwa sasa imehujumiwa na dhana kuwa japo mtu ni mnene jamii haitambagua kwani watu wengi duniani ni wanene'' "Nafikiri kwamba itatubidi tuwaelimishe wazazi kuhusiana na maswala ya afya ya watoto wao na pia kuwaeleza kuwa wanapaswa kufuatilia kwa karibu unene au sio wa watoto wao'' Anapendekeza kuwa sheria madhubuti zinapaswa kutungwa ilikuzima matangazo ya kufana ya vyakula vyenye mafuta mengi.

BBC.