Jumamosi, 28 Februari 2015

AZAM WAJANJA SANA AISEE.

JOPO la viongozi wa Azam FC lililotua hapa Sudan, limeruka vihunzi kadhaa vya hujuma na kufanikiwa kuwaficha wachezaji wao katika moja ya nyumba za kisasa hapa Khartoum wakati Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Juma Nkamia, akiwasili mjini hapa kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ushindi. Azam ilitua Khartoum Jumatano Alfajiri kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh ya hapa mchezo utakaofanyika leo Jumamosi majira ya saa mbili usiku kwa saa za Tanzania. Mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam Azam ilishinda mabao 2-0. Kwa kuhofia hujuma za wenyeji wao waliowaanzishia vitimbi kwa kuwapa gari bovu wakati wanawasili, viongozi wa Azam wamekuwa wakitumia usafiri wao wa binafsi lakini pia wameigomea hoteli waliyopewa na wenyeji na kukodi moja ya nyumba kubwa za kisasa na kuwaficha wachezaji wake ambapo ulinzi umeimarishwa. Katibu wa Azam, Nassoro Idrissa ‘Father’ alisema baada ya kuamua kufanya mambo yao wenyewe kwa kushirikiana na Watanzania wanaoishi hapa Sudan, hali imekuwa shwari na wanaendelea vizuri. “Hakuna hujuma mpaka sasa, tumefanikiwa kuwatafutia wachezaji wetu sehemu nzuri, juzi tumefanya mazoezi katika uwanja wa jeshi, lakini taa zake zimekuwa hazina nguvu sana hivyo leo (juzi Alhamisi usiku) tumeamua kuja kufanyia kwenye huu uwanja huu wa Ratib Nassir,” alisema Nkamia aliyewasili kuwapa nguvu wachezaji wa Azam alifanya mazungumzo mafupi na wachezaji hao mara baada ya kuwasili mjini hapa juzi usiku. Kutokana na hofu ya kuhujumiwa katika chakula, wachezaji wa Azam wamekuwa wakibadilisha sehemu wanazopata chakula mara kwa mara jambo ambalo linafanyika kwa siri sana ili kutotoa mwanya wa kuhujumiwa. Licha ya kwamba Azam imekuwa ikifanya mazoezi kuanzia majira ya saa moja usiku, bado muda huo una joto kali hapa Khartoum kama lilivyokuwa joto la saa nane katika Jiji la Dar es Salaam. Lakini wachezaji hao wameanza kuizoea hali hiyo kutokana na kuwasili mjini hapa mapema. Katika hali ya kushangaza, wakazi wa hapa walifurika katika mazoezi ya Azam juzi na kufuatilia mazoezi hayo mwanzo mwisho huku wengine wakizitafuta jezi za timu hiyo ili wazinunue kwa kuvutiwa nayo. MWANASPOTI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni