Bila shaka msomaji wangu unaendelea vyema na shughuli zako za
ujasiriamali. Mada ya njia za uhakika za kupata mtaji wa kuanzisha
biashara ni ndefu lakini naamini kila siku unajifunza kitu kipya chenye
manufaa makubwa kwako.
Leo nataka kujadili nawe njia mpya ya kupata mtaji wa kuanzisha
biashara ambayo naamini hata wewe unayelalamika kila siku kwamba huna
mtaji, inaweza kukusaidia kujikwamua kutoka hapo ulipo.
TUMIA PESA YA MTEJA KUANZISHA BIASHARA YAKO
Unaweza kupata mtaji
kwa kufikiri kwa utofauti na watu wengine. Katika njia hii ambayo
kijasiriamali huitwa Customer Financing, mteja hukupatia pesa kwa ajili
ya wewe kutengeneza bidhaa au huduma anayoihitaji. Kinachohitajika hapa
ni uaminifu wa hali ya juu.
Kuna biashara nyingi ambazo huu ndiyo huwa utaratibu wa uendeshwaji
wa biashara ambapo mteja hutakiwa kulipa kwanza ndiyo bidhaa au huduma
iandaliwe. Mfano, kama una kipaji cha kupika vizuri, unaweza kuanzisha
biashara ya ‘catering’ au biashara ya kulisha watu kwenye matukio ya
kijamii.
Unachotakiwa kuwa nacho ni kujiamini, kutafuta watu wenye uhitaji na kuwaambia kuhusu biashara yako.
Mteja akikubali atakulipa kabisa na utakachotakiwa kukifanya ni
kukodisha vyombo, kukodi wapishi na kununua vyakula kwa ajili ya
maandalizi ya shughuli husika kama mchele, nyama, mafuta nk. Baada ya
hapo itatakiwa utafute wahudumu wa kukusaidia kugawa chakula na
kuwahudumia wahusika wa shughuli yenyewe.
Jambo la kuelewa hapa ni kwamba mjasiriamali ni mtu anayechanganya
malighali na watu na kutengeneza tija (value) mahali ambapo kusingekuwa
na tija. Kuwa mjasiriamali ni sawa na kuwa mtengeneza filamu ambaye
anatafuta wasanii, eneo la kuchukulia filamu, pamoja na vitendea kazi
vyote.
Baadaye filamu ikiwa tayari sisi hununua kuangalia na kufurahia wakati yeye akiwa ameshaingiza pesa yake.
Mtaji mkubwa hapa huwa ni uamanifu. Hapa kwetu kuna watu wengi
wanakwama kila siku kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa wateja wao. Kwa
mfano wapo baadhi ya wajasiriamali wanaoendesha biashara ya utalii
ambapo kimsingi mteja ambaye yuko Ulaya, Australia, Marekani au Asia
hutakiwa kulipia huduma hiyo kabla hajaja nchini.
Kwa sababu
ya tamaa, wajasiriamali wengi kwenye fani huishia kutumia pesa hiyo kwa
matumizi binafsi na kukosa uaminifu. Mtalii anapofika nchini hupigwa na
butwaa kwa kuona kwamba huduma anayopewa ni ya chini sana tofauti na
malipo na makubaliano ya awali.
Pia ipo mifano kadhaa ya aibu sana kwa taifa letu ambapo mjasirimali
wa soko hili akishalipwa hutokomea kabisa na kumwacha mtalii kwenye
mataa. Mara nyingi baada ya kutua uwanja wa ndege na kujaribu kufanya
mawasiliano na mhusika, ndiyo anapogundua kwamba mjasiriamali ni tapeli.
Matokeo yake wajasiriamali wachache kama hawa huliabisha taifa letu
na kuwaumiza wajasiriamali wengine wa soko la utalii kwa wageni kutilia
mashaka huduma zetu kwa jumla. Hivyo kama utapata mtaji kwa njia hii
hakikisha unakuwa ni mwaminifu na utabarikiwa na kufika mbali maishani.
Kama unataabika na kukosa uaminifu na tamaa huwa inataka kukuharibia
bahati yako kwenye biashara nakushauri upate ushauri wa kitalaamu au wa
kiroho mfano kuwaomba watumishi wa Mungu wakuombee, kwani kama hili ni
tatizo kwako, hata ungeenda juu kiasi gani,utaanguka siku moja kwa kuwa
msingi wako kijasiriamali siyo imara.
Kingine ni kutafuta na kusoma kitabu kinachoitwa The Speed of Trust
cha Stephen M.R Covey ambacho ni moja kati ya vitabu bora kabisa
ulimwenguni juu ya somo na faida nyingi za uaminifu maishani.
Sehemu
nyingine ya wazi ambapo unaweza kutumia pesa ya mteja ni kwenye
biashara za mtandao au Multilevel Marketing au kwa kifupi (MLM).
Makampuni ya mfumo huu ambayo mengi hutokea Marekani, Asia au Ulaya
huwapatia wanachama wake sample za bidhaa zao kwa ajili ya kuwaonesha au
kuwaonjesha wateja wapya.
Kama mteja atavutiwa na bidhaa basi hutakiwa kukupatia pesa ili uweze
kumnunulia bidhaa kutoka kwenye kampuni husika na kumpelekea pale
alipo. Wewe kama mwanachama utaweza kujipatia cha juu (faida) kwani
utanunua bidhaa zile kwa bei ya punguzo (membership price) na kumuuzia
mteja wako kwa bei ya juu ambayo mara nyingi hupangwa na kampuni.
Watu wengi hapa kwetu wamejikwamua kwa njia hii na kuweza kupata
mitaji ya kuendeshea biashara zao binafsi na wengine wengi wameweza
kupunguza makali ya maisha kwa njia hii. Pia wapo wachache ambao
wamekuwa mamilionea kwa kupitia biashara hizi kwa kufanya kazi kwa bidii
sana na kwa muda mrefu bila kukata tamaa.
Wengi wa mamilionea hawa hawakuwa na mtaji wowote walipoanza miaka
michache iliyopita zaidi tu ya kuwa na ujasiri wa kuongea na watu wengi
kadiri walivyoweza na kuwaomba wateja walipie kwanza bidhaa
wanazozihitaji na kuzipokea baadae.
Kama wewe ni mtu unayependa kujichanganya na watu wengine (social),
unaweza kujituma na kujisimamia mwenyewe (self motivation) huogopi
kukataliwa (rejection) na hukati tamaa kirahisi, basi biashara hii
inaweza kukufaa zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni