Katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa kwenye tunda la chungwa, iligundulika kwamba tunda hili lina uwezo mkubwa wa kuponya matatizo mbalimbali ya kiafya kwa sababu lina mkusanyiko mkubwa wa virutubisho vya Phytonutrients. Jamii ya virutubisho hivyo inajumuisha pamoja na citrus flavanones, anthocyanins, hydroxycinnamic acids na polyphenols, ambapo inaelezwa kwamba virutubisho hivyo vinapochanganyika na Vitamin C inayopatikana kwenye chungwa, uwezo wake wa kutoka kinga mwilini huwa mkubwa. Moja ya faida nyingi za virutubisho hivyo ni pamoja na kushusha kiwango cha shinikizo la damu pamoja na kiwango cha mafuta mabaya mwilini, maarufu kwa jina la Kolestro. Jambo la muhimu kuzingatia sana hapa ni kwamba virutubisho vingi muhimu vinapatikana kwenye maganda na nyama nyeupe ya chungwa na siyo kwenye maji peke yake. Kwa maana nyingine ili upate vitamini na virutubisho vyote muhimu vinavyopatikana kwenye tunda la chungwa, inashauriwa kulila pamoja na nyama zake, na siyo kukamua maji peke yake. Ingawa wa kufanya hivyo bado una uhakika wa kupata Vitamin C ambayo ndiyo inapatikana kwa wingi kwa kunywa juisi yake tu.
UNAUJUA UMUHIMU WA VITAMIN C ?
Bila shaka utakuwa unaelewa tangu zamani kwamba chungwa ni chanzo kikubwa cha Vitamni C, kwani chungwa moja lina uwezo wa kutoa hadi asilimia 116 ya kiwango kinachotakiwa kwa siku, lakini pamoja na kujua hilo, unafahamu Vitamini C na machungwa kwa ujumla ni muhimu kiasi gani katika afya yako? Kwanza kabisa Vitamini C hutoa kinga ya mwili kupambana na maradhi kama vile mafua, kikohozi na hata kifua kikuu na vile vile huondoa vijidudu nyemelezi (free radicals) mwilini na kuzipa seli kinga madhubuti ya kutoharibika, nje na ndani. Inaelezwa kwamba hatari kubwa ya kwanza seli inapokuwa haina kinga dhidi ya vijidudu nyemelezi, ni kupatwa na saratani, hasa ya utumbo. Lakini ukiwa na Vitamni C ya kutosha mwilini, unakuwa umejitengenezea kinga madhubuti dhidi ya saratani hiyo. Aidha seli zinapokuwa zimedhurika kwa kukosa kinga, mwili mzima huwaka moto kwa maumivu, hasa wakati mwili unapokuwa ukijaribu kuondoa seli zilizodhurika. Hivyo inaelezwa kwamba Vitamin C, ambayo ndiyo huzuia vijidudu nyemelezi vinavyosababisha maumivu ya mwili kuongozeka, hutoa nafuu zaidi kwa magonjwa hayo na mengine kama pumu na viungo. Vilevile vijidudu nyemelezi (free radicals) ndivyo vinavyosababisha kuganda kwa kolestro mwilini ambapo inapofikia hali hiyo husababisha kuziba kwa mishipa ya damu na mwisho huleta mshituko wa moyo au kiharusi. Lakini kwa mwili kuwa na Vitamin C ya kutosha, hali hiyo haiwezi kutokea kwani Vitamin hii ina uwezo wa kudhoofisha vijidudu hivyo visilete uharibifu.
GLASI MOJA YA JUISI NI BORA KULIKO VIDONGE
Utumiaji wa vidonge vya Vitamin C hauwezi kutoa faida za kinga sawa kama kunywa glasi moja ya juisi halisi ya machungwa, hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kitengo cha Virutubisho vya Binadamu cha Chuo Kiuu cha mjini Milan, Italia. Hii ina maana kwamba ukinywa juisi halisi ya machungwa utapata faida za kinga zaidi kuliko kula vidonge vyake (food supplements). Kwa kutambua faida za kiafya zinazopatikana kwenye Vitamin C, si jambo la kushangaza kuambiwa na watafiti wetu kwamba ulaji wa matunda na mboga zenye kirutubisho hicho kwa wingi, vina uhusiano mkubwa wa kupungua, kwa kiasi kikubwa, kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa wa moyo, kiharusi na saratani. (Heart Disease, stroke and cancer).
CHUNGWA CHANZO KIZURI CHA 'FIBER'
Faida za kiafya za chungwa zingali zikiendelea hadi kwenye kirutubisho kingine kinachojulikana kama 'fiber' au ufumwele. Tunaelezwa kwamba chungwa moja tu hutoa asilimia 12.5 ya kiwango cha ufumwele kinachotakiwa kwa siku katika mwili wa binadamu, kirutubisho hiki kimeonesha uwezo mkubwa wa kupunguza mafuta mabaya mwilini (cholestro). Vile vile ufumwele unasifika kwa kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, hivyo chungwa ni tunda muhimu kwa wangonjwa wa kisukari, hasa wanapokula pamoja na nyama yake. Kwa kuongezea, sukari ya asili inayopatikana kwenye chungwa (fructose), inaweza kusaidia kudhibiti kupanda kwa kiwango cha sukari mara baada ya mgonjwa kula chakula. Vile vile ufumwele unaopatikana kwenye chungwa una uwezo wa kuondoa viwakilishi vinavyosababisha saratani ya utumbo kwa kutoa utandu wa kinga kwenye tumbo. Mbali na hilo, machungwa pia hutoa nafuu kwa watu wanaosumbuliwa na tumbo au ugonjwa wa kuharisha. Kula chungwa na nyama yake ili upate faida zote zinazopatikana kwenye virutubisho vilivyomo kwenye tunda hilo.
CHUNGWA HUONDOA MAWE KWENYE FIGO (Kidney stones).
Kama unataka kujikinga na ugonjwa wa kupatwa na mawe kwenye figo, basi unashauriwa kunywa juisi ya machungwa! utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa kwenye jarida la masuala ya lishe la Uingereza (British Journal of Nutrition), uligdundua kwamba wanawake walipokunywa nusu lita mpaka lita moja ya juisi ya machungwa au zabibu kila siku, usafishaji wa njia ya mkojo uliongezeka hivyo kuondoa kabisa hatari ya kuwa na mawe kwenye figo (calcium oxalate stones).
CHUNGWA HUTOA KINGA DHIDI YA VIDONDA VYA TUMBO.
Chungwa moja kwa siku, linaweza kukusaidia kukupa kinga dhidi ya vidonda vya tumbo, hii ni kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Chuo cha Lishe cha nchini Marekani ambapo zaidi ya watu wazima 6000 walifanyiwa utafiti kuthibitisha hilo. HITIMISHO Kwa ujumla, hizo ni faida chache tu na muhimu zinazopatikana kwenye tunda hili, lakini kuna faida nyingine nyingi tu. Kimsingi tunashauriwa kula matunda ya aina mbalimbali kwa wingi kadri tuwezavyo, kwani kwa kufanya hivyo tutajihakikishia upatikanaji wa faida zote za kiafya zilizomo kwenye matunda. Kwa kula matunda mengi na mchanganyiko, ndiko kunakoweza kukupa kinga ya mwili na afya njema iliyohuru na maradhi sugu kama vile ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, kiharusi, kisukari, n.k. Mungu ametupa matunda mchanganyiko yanayopatikana mwaka mzima katika vipindi tofauti, kwa sababu maalum. Hivyo ni kosa kubwa sana kuacha kutumia matunda haya ya msimu kila yanapopatikana na ni makosa makubwa kiafya kujenga tabia ya kutokula tunda la aina yoyote hata kwa mwaka mzima. Kuanzia leo anza kulithamini chungwa na kuliona kama mkombozi wa afya yako.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni