Rais Kenyatta aliidhinisha sheria hiyo akisema itaisaidia Kenya kudhibiti hali ya usalama
Wakili wa serikali Njoroge Mwangi amesema serikali itakata rufaa
Sheria hiyo tata ilipitishwa bungeni tarehe 14 Desemba mwaka uliopita katika kikao kilichokumbwa na vurumai huku wabunge wakipigana hadharani.
Baada ya hapo Rais Uhuru Kenyatta alitia saini mswada huo na kuufanya sheria tarehe 22 mwezi huo kisha chama cha CORD kikakwenda mahakamani kikidai kuwa sehemu nyingi za sheria hiyo zilikiuka katiba.
Mashirika mengine yalijiunga katika mchakato huo na kujumuishwa katika kesi ikiwemo tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu.
Awali jaji wa mahakama kuu alikuwa amezuia vipengele vinane vya sheria hiyo kutotekelezwa na kumchochea mkuu wa sheria kukataa rufaa lakini bado mahakama ya rufaa ikashikilia uamuzi wa mahakama kuu.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni kutazama mwelekeo utakaochukuliwa kwa misingi kuwa CORD inasema itaenda kwa mahakama ya rufaa vile vile kutaka sehemu nyingine za sheria hizo kuchunguzwa.