Jumamosi, 21 Februari 2015

MATUKIO YA KISIASA.

Matukio ya Kisiasa

Rais wa zamani wa Yemen atoroka kifungo cha nyumban Rais wa zamani wa Yemen Jumamosi (21.02.2015) ametoroka kutoka kifungo cha nyumbani cha wiki kadhaa mjini Sanaa nyumba yake ikiwa imezingirwa na waasi wa Kishia Washauri walio karibu naye wamesema kwamba Rais huyo wa zamani Abd Raboo Mansour Hadi ameondoka Sanaa na tayari amewasili katika mji mkuu wa iliokuwa Yemen ya kusini Aden ambapo wafuasi wake wamegoma kuyatambuwa mamlaka ya baraza la rais lililowekwa na wanamgambo wa Kihouthi kuchukuwa nafasi yake. Ameondoka mjini Sanaa akiwa kwenye msafara wa magari kadhaa kwa kupitia mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo wa Taiz ambao kama vile Aden hauko chini ya udhibiti wa waasi wa Kishia wa kundi la Wahouthi. Afisa mwandamazi wa uslama mjini Aden ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Hadi mwenye umri wa miaka 69 anakaa kwenye kasri la rais katika kitongoji cha kidiplomasia cha mji huo wa bandari wa Yemen kusini ambako ndiko alikozaliwa. Aliwababaisha walinzi Washauri wake wanasema kwamba Hadi ambaye amekuwa kwenye kifungo cha nyumbani kwa wiki kadhaa kufuatia mapinduzi ya waasi hao wa Kishia anapanga kuondoka nchini kwenda nje kwa ajili ya matibabu. Washauri hao wameongeza kusema kwamba waasi wamemuachia Hadi kutokana na shinikizo kutoka Umoja wa Mataifa,Marekani,Urusi na vyama kisiasa ndani ya nchi hiyo. Hata hivyo mjumbe wa kamati kuu ya kundi la Wahouthi Ali al-Quhum ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba Hadi alitoroka kifungo hicho cha nyumbani kwa kuwakwepa walinzi kwa kuwababaisha. Afisa huyo mwandamizi pia amekaririwa akisema hayo na tovuti ya habari ya ndani ya nchi ya al-Akhbar na kuongeza kwamba hakuna tena maana iwapo rais huyo wa zamani ameendelea kubakia hapo au kuondoka. Wahouthi walivyodhibiti serikali Wanamgambo wa kundi la Wahouthi ambao ngome yao kuu iko nyanda za juu kaskazini wanakoishi Washia wengi waliuteka mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa hapo mwezi wa Septemba bila ya upinzani.Mwezi uliopita waasi hao waliiteka Ikulu na kuyazingira makaazi ya Hadi jambo lililopelekea rais huyo kujiuzulu. Kwa mujibu wa mashahidi baada ya Hadi kuondoka kwenye makaazi yake Wahouthi walifanya uporaji kwenye nyumba yake na kwamba watu watatu walionekana wakitoka na bunduki za aina ya Kalashnikov kutoka kwenye nyumba hiyo. Jamal Benomar mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen amesema hapo Ijumaa kwamba makundi yanayohasimiana nchini humo yamekubaliana kuunda baraza jipya la kutunga sheria litakalojumuisha Wahouthi, wabunge wa zamani na wapya kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito. Lakini muungano wa vyama vya kisiasa nchini humo umeukataa mpango huo kwa hoja kwamba haukidhi haja ya kuleta ufumbuzi kamili. Ahmed Lakaz msemaji wa chama cha Mkusanyiko wa Vyama vya Wafanyakazi ambacho kilikuwa kinashiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Yemen amesema kwamba vyama hivyo vimewaeleza Wahouthi kwamba hawatashiriki katika mchakato huo iwapo Hadi hatoachiliwa. Kutumbukia kwenye mzozo wa kisiasa Yemen imetumbukia kwenye mzozo wa kisiasa tokea waasi wa kundi la Wahouthi kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa na baadae kulazimisha kujiuzulu kwa rais aliyechaguliwa anayeungwa mkono na mataifa ya magharibi na kulivunja bunge wakati wakimweka Hadi kwenye kifungo cha nyumbani. Wakati huo huo waasi hao wa kundi la Wahouthi Jumamosi walijaribu kuvamia kambi ya kikosi maalum ilioko nje ya mji mkuu na kushambuliana kwa risasi na wanajeshi wa kikosi hicho ambao wengi wao ni tiifu kwa Ali Abdallah Saleh mtangulizi wa Hadi.Kwa mujibu wa maafisa wa usalama mapigano hayo yameuwa watu watatu. Washauri wa Saleh wanasema kiongozi huyo wa zamani anaiona kambi hiyo kuwa muhimu kwa uhai wake na kamwe hatoruhusu iangukie mikononi mwa Wahouthi kama vile ilivyokuwa kwa vituo vyengine vya kijeshi ambavyo tayari viko mikononi mwa Wahouthi. Washauri wake hao wamezungumza hayo kwa masharti ya kutotajwa jina kutokana na kwamba Saleh hakuwaruhusu wazungumze na waandishi wa habari. Maandamano dhidi ya Wahouthi yaendelea Maelfu ya watu pia wameandamana Jumamosi kumuunga mkono Hadi katika mji wa kusini wajimbo la Ibb ambapo wamewataka Wahouthi kuondoka katika eneo hilo na kuacha kuingilia kati masuala ya ndani ya jimbo hilo.Duru za usalama zinasema Wahouthi waliwafyetulia risasi na kuuwa mwandamanaji mmoja na kujeruhi wengine wawili. Waasi hao wa kundi la Wahouthi walijipenyeza hadi kwenye maeneo yanayokaliwa na Wasunni wengi kusini na magharibi mwa mji mkuu wa Sanaa ambapo walikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa kikabila na wanamgambo wa kundi la Al Qaeda. Mji wa Taiz na baadhi ya sehemu nyengine za kaskazini halikadhalika eneo zima la kusini mwa Yemen hayako chini ya udhibiti wa waasi hao. Mzozo huo wa kisiasa nchini Yemen pia unauweka mashakani uwezo wa Marekani kuendeleza operesheni zake za kupambana na ugaidi hususan kutokana na kuondolewa kwa Hadi mshirika madhubuti wa Marekani. IDHAA YA KISWAHILI DW.DE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni