Jumamosi, 21 Februari 2015
RIPOTI JUU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI YATOLEWA
Ripoti juu ya uhuru wa vyombo vya habari yatolewa
Kila mwaka shirika hilo la waandishi wasio na mipaka lililo na makao yake mjini Paris Ufaransa, linafanya uchunguzi kwa mataifa 180 ili kuangalia hali ya uhuru wa vyombo vya habari. Kulingana na Christophe Deloire, Mkuu wa shirika hilo, kumekuwa na ongezeko la asilimia 8 ya ukiukwaji wa uhuru huo mwaka wa 2014.
Hii ikimaanisha kumekuwepo na visa 3,719 vya ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari katika mataifa 180 mnamo mwaka huo.
Christophe Deloire amesema hali hiyo imesababishwa na makundi ya wanamgambo kama vile dola la kiislamu walioko nchini Iraq na Syria pamoja na wanamgambo wa Boko Haram walioko Nigeria wanaozuia ujumbe unaofika kwa vyombo vya habari au kwa kuwateka nyara na kuwauwa baadhi ya waandishi walio chini ya udhibiti wa kundi hilo.
Kuongezeka kwa ghasia dhidi ya wanahabari katika maandamano tofauti duniani pia kumechangia kudorora kwa uhuru wa vyombo vya habari lilisema shirika hilo la waandishi wasio na mipaka, likitolea mfano kukamatwa kwa waandishi 15 walipokuwa wanafuatilia maandamano ya kupinga mauaji ya Kijana mweusi wa kimarekani Michael Brown aliyepigwa risasi na polisi mweupe Katika eneo la Ferguson, Missouri.
Kwa upande mwengine hatua ya serikali kufungia vyombo vya habari kwa kisingizio cha kulinda usalama wa Kitaifa pia imechangia kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari.
Rwanda yazidi bado inabana uhuru wa vyombo vya habari
Finland Norway na Denmark ndio mataifa yaliowekwa katika nafasi tatu za kwanza kama mataifa ambayo angalau uhuru wa vyombo vya habari unaheshimika huku nafasi tatu za mwisho zikiiangukia Eritrea, Korea Kakazini na Turkmenistan.
Tanzania imewekwa katika nafasi ya 75, Uganda nafasi ya 97 huku Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zikishikilia nafasi ya 100 na 107 Nigeria imejipata katika nafasi ya 111 Burundi 145 na Rwanda ikiwa katika nafasi ya 161 hii ikimaanisha Uhuru wa vyombo vya habari katika nchi hizi bado zinakabiliwa na changamoto kubwa.
Tukiangalia mataifa yalio katika migogoro kwa mfano katika maeneo ya Mashariki ya kati na hata Ukraine shirika hilo limesema waandishi wa habari wamelengwa kwa kuuwawa au kulazimishwa kuandika habari za propaganda, na hata kuwalenga wanablogu ambao wanachunguza masuala tofauti yanayofanywa na serikali au watu binafsi.
Marekani katika ripoti hiii imeshuka nafasi tatu chini na kujipata katika nafasi ya 49 sababu kubwa ikiwa vita vya marekani dhidi ya Wikileaks mtandao unaotoa habari kwa Umma. Urusi imeshika nafasi ya 152 kwenye orodha hiyo huku Ukraine ikiwa mbele kidogo katika nafasi ya 129.
IDHAA YA KISWAHILI DW.DE
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni