Jumapili, 8 Februari 2015

UTAJIRI UPO MAWAZONI, SIYO MDOMONI

NIMEKUWA nikisema hapa mara kwa mara jinsi gani mtu anaweza kubadili maisha yake kuanzia sifuri hadi kuwa mwenye mafanikio makubwa. Nimewahi pia kutoa mifano mbalimbali ya watu ambao maisha yao yalianzia chini kabisa na sasa ni matajiri wa kuogopwa.

Nitaendelea kukumbusha wajibu wako kama mtu unayesaka mafanikio na leo nakuambia kuwa mabadiliko yoyote ya kimaisha yanaanzia mawazoni mwako, tofauti na wengi ambao hudhani wanaweza kuyafikia kupitia midomo yao.

Kama kweli unasaka mafanikio, ni lazima moto fulani wa njaa ya utajiri uwe unawaka mawazoni mwako na ili kujua kama moto huo upo, yakupasa kujiuliza maswali kadhaa wa kadhaa.

Hivi unayo picha ya aina ya gari na nyumba ambayo unataka kuwa nayo bapo baadaye?  Vipi, unafanya juhudi zozote za kujiongezea kipato chako? Unafanya kazi kwa kiwango cha juu na hulali mapema kwa ajili ya kazi, unajaribu kufanya vitu vipya kila siku?

Watu wengi wana ndoto za kuwa matajiri lakini hawataki kuwa matajiri. Unatakiwa kuachana na simulizi za mdomoni na badala yake uwe na msukumo wa dhati moyoni mwako kwa ajili ya kusonga mbele katika malengo yako.

Kama kweli unataka kuwa tajiri, basi ni lazima uwe siyo mtu wa kulala mapema kwa mawazo, kufanya kazi zaidi, kuwa tayari kukabiliana na hofu yoyote mbele yako, uwe mtu ambaye uko tayari kubahatisha, kuwa tayari kujitoa muhanga na kukabiliana na changamoto zozote zinazojitokeza katika njia yako.
Ni kwa kufanya hivyo tu, njia ya kuufikia utajiri iko wazi mbele yako.

Fikiria kama mtu hujala siku tatu mfululizo, njaa yako itakuuma kiasi gani? Ni vipi kama kula yako itapatikana endapo tu utatakiwa kumuua mnyama? Kwa vyovyote utakuwa tayari kupambana na mnyama huyo ili ule, na huo ndiyo mfano halisi wa hamu ya kuwa tajiri inavyotakiwa kuwa mawazoni mwako.

Watu wote ambao walikuja kuwa matajiri walikuwa wakifikiri kwa namna moja na baadhi ya kauli kama hii inathibitisha aina yao ya ufikiriaji, “Siwezi kupumzika hadi niwe tajiri”







Watu wanaweza kupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa sababu siku zote wanasema siyo busara kutegemea chanzo kimoja tu cha mapato, wakati huku ukiwekeza katika miradi mbalimbali, ni vyema pia kuwa na vitu vingine kama biashara ya elimu ya ujasiriamali kwa wenzako.

Wapo watu wengi ambao wangependa kufanya ujasiriamali, lakini bahati mbaya hawana uelewa wa nini cha kufanya. Kama unayo elimu hiyo, unaweza kufungua darasa na kujikuta ukijiongezea kipato kwa kutoa elimu hiyo kwa wenzako. Kila mara akili yako iende katika kuongeza kipato zaidi na zaidi ya kile ulichonacho leo.

Uelewa wa jambo lolote, uwe unalifanya au haulifanyi, ni kitu kimoja cha msingi sana kwa sababu kuna kauli mbiu inasema, uelewa siyo tu ni nguvu, bali ni pesa. Wekeza sana katika uelewa, jitahidi kusoma, hudhuria kozi, sikiliza vipindi na soma kadiri unavyoweza.

Na kumbuka kanuni moja ya msingi, uelewa unaweza kuuzwa moja kwa moja kwa fedha au ukatumika kwa namna nyingine kukupatia fedha kutoka kwa vyanzo vingine.

Hata mwizi hutumia uelewa wa jinsi ya kufungua milango na madirisha yaliyofungwa, namna gani atapita bila kuonekana na pia anajua njia ya kupita ili asikamatwe, sikufundishi kuwa mwizi, lakini ninachotaka uelewe ni kuwa kila mtu anayeingiza fedha anafanya hivyo kwa sababu ana aina fulani ya uelewa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni