Jumamosi, 28 Februari 2015

TUMEPITA.

KIPATO huleta majivuno. Ni usemi maarufu wa Kiswahili unaoweza kutumika kutafsiri kipigo cha mabao 2-1 ilichopata ugenini dhidi ya BDF XI kwenye mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho. Lakini hiyo haiondoi Yanga kuitwa Wanaume wa Shoka kutokana na ugumu wa michuano hiyo. Yanga ilishinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa awali jijini Dar es Salaam, matokeo yaliyoipa kiburi kiasi jana Ijumaa ikacheza kwa mbwembwe zilizosababisha matokeo hayo ingawa mwamuzi naye alitoa kadi za njano ambazo ziliwapa mchecheto wachezaji wa Yanga. Hata hivyo imesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 ikibebwa na ushindi wake wa kwanza. Yanga ilitumia sekunde 1800 ambazo ni dakika 30 kupata bao la kuongoza lililofungwa kwa kichwa kupitia kwa kiraka mwenye kasi Mrisho Ngassa ambaye alipokea pasi ya Amissi Tambwe aliyeituliza kwenye boksi krosi safi ya Msuva. Bao hilo liliwachanganya wenyeji ambao kipindi chote cha kwanza hawakupiga hata shuti moja la maana. Kipindi cha pili ambacho wachezaji wa Yanga walionekana kuzidiwa na hali ya hewa ya baridi, Moreetsi ‘Resco’ Mosimanyana aliipatia bao BDF dakika ya 46 kupitia krosi ya Pelontle ‘Dust’ Lerole ambayo ilimshinda kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyeonekana kusumbuliwa na mipira ya juu hususani kipindi cha pili. Dakika ya 69 Danny Mrwanda alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kucheza rafu mbaya. Kutolewa kwake kuliwapa nguvu wenyeji na dakika ya 85, Kumbulani Madziba aliyewachambua mabeki wa Yanga na kuuminya kiulaini langoni kuandika bao la pili. Yanga iliyowasimamisha viungo imara; Twite, Haruna Niyonzima na Ngassa, ilikosa mabao matatu ya wazi kipindi cha kwanza kupitia kwa Tambwe, Mrwanda na Ngassa huku wenyeji wakipata hasara dakika ya 20 baada ya beki wao Othusitse ‘Nakata’ Mpharithe kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Msuva. BDF ambayo walikuwa wakifaidi maumbo yao marefu, hususani kwenye mipira waliyokuwa wakitanguliziwa mawinga wafupi wa Yanga, walicheza mpira wa taratibu huku wakishindwa kuendana na mbwembwe za Yanga ambayo kocha wake Hans Pluijm alionyesha uzoefu wa kimataifa kwa kuwatuliza wachezaji wakacheza bila mchecheto. Yanga ambayo ilitumia bajeti ya Sh168 milioni kwenye mechi mbili, ile ya Dar es Salaam na ya jana, ilianzisha kikosi chenye watu wenye kasi ambacho kilisaidia mashambulizi ya kushtukiza kwa kuwatumia Msuva, Ngassa na Mrwanda. Yanga sasa itacheza mchezo wa raundi ya kwanza Machi 14 na mshindi wa mechi ya leo Jumamosi baina ya Sofapaka ya Kenya na Platinum ya Zimbabwe mchezo utakaochezwa mjini Harare. Katika mechi ya kwanza jijini Nairobi, Sofapaka inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Sam Timbe ilifungwa mabao 2-1. Mechi hiyo itachezeshwa na Mbotswana, Tirelo Mositwane. Mashabiki Awali mashabiki zaidi ya 100 wa Yanga waliotoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani walikwama kuingia Botswana kuangalia mechi hiyo baada ya kuzuiwa mpakani mwa Zambia kwa kuwa hati zao za kusafiria ni za karatasi. Kwa mujibu wa maofisa wa uhamiaji wa eneo hilo, pasi hizo haziruhusiwi bali zile za vitabu ndizo halali za kuingilia kwenye nchini hiyo. Chakula na Basi Chakula cha mchana wachezaji wa Yanga walikula kwenye hoteli tofauti na ile waliyofikia na wakati Yanga inaondoka pia hotelini kwenda uwanjani ilibadili basi ambapo lile lililokuwa limeandaliwa na wenyeji kwaajili ya kutumiwa na wachezaji likapandwa na mashabiki na wachezaji wakakodiwa basi jingine na uongozi. Pondamali aachwa Katika tukio ambalo liliibua maswali mengi, Yanga walipoondoka hotelini walimsahau kocha wao wa makipa, Juma Pondamali ambaye walilazimika kumkodia usafiri maalum ili awahi mchezo huo. Zawadi Yanga ikipenya kwenye mechi sita zilizobaki ina uhakika angalau wa dola 150,000(Sh267 milioni). MWANASPOTI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni