Alhamisi, 5 Machi 2015

KABURU AMWAGA MBOGA SIMBA.

MAKAMU wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, ameitumia Mwanaspoti kuwaambia maelfu ya mashabiki wa Simba yaliyo moyoni mwake kuhusiana na mwenendo mbovu wa timu hiyo na tuhuma zinazoelekezwa kwake. Kaburu ametamka kwamba anashangazwa na kauli nyepesi zinazotolewa na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya klabu hiyo wakimtoa kafara kuwa yeye ndiye mhusika mkuu wa kuhujumu timu, lakini wanasahau kuwa robo tatu ya wachezaji ndani ya timu yao ni vijana ambao hawana uzoefu. “Mimi ni Makamu wa Rais nihujumu timu ili iweje? Nipate faida gani? Aveva (Evans) ni Rais, anatakiwa kuacha kusikiliza majungu na atoe maelezo sahihi kwa wanachama juu ya kinachoendelea ndani ya klabu kwa sasa,” alisema Kaburu. “Aseme ni kwa nini tumefika hapa si kutoa majibu mepesi, mimi sina ugomvi na kiongozi yeyote, lakini baadhi ya viongozi wenzangu ni wazandiki. “Timu yetu ni mpya, robo tatu ya wachezaji ni vijana na hawajakaa pamoja kwa muda mrefu, kocha tuliyenaye pia ni mpya, tulikosea kwenye usajili tulidhani kusajili chipukizi kutasaidia timu, lakini tukasahau linapofika suala la mashindano, uzoefu unasaidia. “Hatukujua tutapata upinzani mkali kiasi hiki kwenye ligi. Timu zimesajili vizuri, zimejiandaa vya kutosha, kuna timu zina wachezaji hawana majina (si maarufu) kama Stand United, lakini ni wachezaji wazuri waliokuwa pamoja muda mrefu na wamezoeana. “Kama tumeamua kujenga timu, basi tujenge timu. Mapungufu yaliyopo yatuongoze katika kutengeneza timu nzuri, si kuendeleza majungu yasiyo na msingi. “Mwaka 2011 Simba haikua na kikosi kizuri, lakini ilikuwa na wachezaji wazoefu na walituwezesha kuchukua ubingwa na tukacheza na Al Shandy, sasa wakiulizwa kwa nini timu inafanya vibaya wanatoa majibu mepesi mepesi tu, eti Kaburu anahujumu timu, ili iweje? “Kunatakiwa kuwe na dhana ya uwajibikaji, kila mtu afanye kazi kwa uadilifu na ajue majukumu yake, kuna Kamati ya Mashindano, badala ya kueleza matatizo ya timu wanasema ni Kaburu, mimi ni Makamu Rais, kamati ninayoingoza ni ya fedha, siwezi kufanya kazi za kamati nyingine.” Kaburu ni kiongozi mwenye urafiki mkubwa na zaidi ya asilimia 80 ya wachezaji wa Simba. Kumpangia kikosi kocha Moja ya shutuma dhidi yake ni kuwa huwa ana tabia ya kumpangia kikosi kocha, Goran Kopunovic. Kuhusu hilo, anasema: “Sijawahi kumpangia kocha kikosi, kwa maneno haya haya tuliitisha kikao cha Kamati ya Utendaji na kocha aliulizwa kama huwa nampangia kikosi au kuna kiongozi anampangia kikosi, kocha alikanusha akasema hapana. “Nakiri nina upungufu wangu wa kibinadamu, lakini sijafikia hatua ya kuhujumu timu yangu, kumpa kocha ushauri naamini si jambo baya. “Nilishafanya hivyo, kwa mfano alimpanga Okwi (Emmanuel), Dan Sserunkuma na Elius Maguli mbele, katikati tukawa tumezidiwa. Nilimshauri Okwi akipanda ni mzito kushuka na akishuka ni mzito kupanda, hivyo aangalie namna ya kuwapanga. Ni ushauri tu, hapo tayari nimeonekana tatizo.” Ukata “Simba kweli kuna ukata wala si siri, vyanzo vya fedha vilivyopo ni kutoka kwa wadhamini wa Ligi (Vodacom), wadhamini wa klabu (Kilimanjaro Lager), Haki za Televisheni (Azam Media), michango ya wanachama pamoja na mapato ya mlangoni,” anasema. “Ili tukidhi mahitaji, tunategemea zaidi mapato ya mlangoni ambayo yamepungua kwa asilimia 60 tena si kwa Simba tu, bali kwa klabu zote za Ligi na tayari Bodi ya Ligi imeshaongea na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kulalamikia mfumo wa elektroniki nao wanazungumza na benki ya CRDB kuangalia namna ya kuuboresha au kuusimamisha mfumo huo, maana tunapoteza mapato mengi. “Kitu kingine kinachochangia ukata ndani ya klabu yetu ni kufanya vibaya kwa timu kiasi cha kushusha morali ya mashabiki kuja uwanjani, pia kuna makato mengi, ndiyo maana fedha inayoingia klabuni ni ndogo. “Inabidi viongozi tutoe fedha mifukoni, hivyo kuna mambo mengine tunashindwa kufanya kwa sababu hatuna fedha. “Lakini tumejitahidi kulipa mishahara ya wachezaji, pia timu yetu ya vijana inashiriki Ligi ya Wilaya na tunaihudumia lengo letu ipande daraja la pili.” Ufafanuzi wa Kaburu umekuja kukiwa na taarifa kuwa amepigwa stop na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo chini ya Aveva kujihusisha na masuala ya timu ikiwa ni pamoja na kutothubutu kukanyaga kwenye kambi ya wachezaji na kumuingilia kocha majukumu yake ingawa Kaburu amekanusha madai hayo.

GAZETI MWANASPOTI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni