Alhamisi, 5 Machi 2015

YANGA YAMPATA MGANGA WA 2-0.

IMANI na juhudi zina mchango mkubwa kwenye mafanikio ya kiumbe hai. Yanga wamekaa chini wakapiga hesabu zao wakaona kwamba kupigia tizi jijini Dar es Salaam kutawalostisha bora waende zao Pwani. Kwa sasa kikosi cha Yanga kinajifua katika Uwanja wa Chuo cha Uvuvi, Mbegani, Bagamoyo uwanja wa mwisho ambao Yanga ilifanyia mazoezi ilipoichapa Simba mabao 2-0, baada ya hapo imekuwa ikiambulia sare au kupoteza mchezo. Wametathmini rekodi za matokeo yao walipokuwa wakitokea kwenye uwanja wanaopenda kuutumia wa Boko Veteran uliopo Bunju Dar es Salaam wakaona mambo yanaweza kuwaendea vibaya. Wazee wakashauri vijana waende Bagamoyo ambako kila wakiweka kambi eneo hilo, Mnyama au timu yoyote ile hachomoki. Kambi hiyo ni Mbegani ambako mara ya mwisho Yanga ilipoweka maskani eneo hilo Mnyama alikula mbili kavu. Kabla ya mchezo huu, Yanga ilicheza michezo miwili dhidi ya Simba kuanzia ule wa Mtani Jembe uliopigwa Desemba 13 mwaka jana ambao timu hiyo ililala kwa mabao 2-0 na mwingine wa ligi uliomalizika kwa suluhu na baadaye wakacheza mechi nyingine ngumu dhidi ya Azam FC Desemba 28 na mchezo ukamalizika kwa sare ya mabao 2-2. Zote hizo walijifua katika Uwanja huo Boko Veteran. WAZEE KAMBINI Kambi hiyo ya Yanga ipo chini ya wazee watatu ambao wamejitolea kuongeza nguvu kuhakikisha kwamba wanashinda. Wanahusika katika kusimamia safari na njia za kupita kwa timu yao ambao kwa pamoja wamesema kazi yao ni kuhakikisha mambo yanaenda sawa. “Nikwambie kijana wangu, hapa wamekuja uwanja wa ushindi hatutaki kuongea sana, kazi hii tumepewa na uongozi kuhakikisha kwamba tunafuta hii hali ya timu yetu kupoteza kwa Simba,” alisema mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mtanange. KOCHA ANENA Kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm alisema: “Tumekubaliana na wachezaji wote kwamba ushindi ni lazima safari hii, najua kwamba watu wana wasiwasi juu ya mchezo huu, tupo tayari kwa vita, naijua Simba kwa sasa, siwezi kusema lolote juu ya ubora wao wala upungufu wao, nitakuwa kama nawaamsha lakini nataka ieleweke kwamba tuna kikosi cha ushindi.”

GAZETI MWANASPOTI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni