Jumanne, 3 Machi 2015
KOMBA AZIKWA NA TINGATINGA.
Nyasa. Safari ya mwisho ya mbunge wa Mbinga
Magharibi jana ilihitimishwa saa 9.25 alasiri
wakati mwili wake ulipofunikwa na mfuniko
mkubwa wa zege uliobebwa na gari maarufu
kwa jina la “kijiko”.
Haikuwa kitu cha kawaida wakati gari hilo
kubwa likishusha mfuniko huo wa zege kwenye
kaburi la mwimbaji huyo maarufu wa nyimbo
za uhamasishaji za CCM na kiongozi wa kundi la
Tanzania One Theatre (TOT), lakini majonzi
yaliwafanya waombolezaji kulichukulia tukio
hilo kuwa la kawaida.
Safari ya Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita
kwenye kijiji cha Lituhi ambako aliazikwa jana,
ilikamilishwa kwa salamu mbalimbali ambazo
zilielezea ushupavu wa kapteni huyo mstaafu
wa jeshi.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya
wananchi, wakiwamo viongozi
mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya
Kikwete na mkewe Salma, yalifanyika katika
makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi
(Bundi) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Nyuso za majonzi zilitawala kwa waombolezaji
waliojitokeza nyumbani kwa marehemu,
takriban mita 500 kutoka katika makaburi hayo
na baadaye katika misa iliyofanyika kwenye
uwanja wa Shule ya Msingi ya Lituhi,
ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo
Katoliki la Mbinga.
Kaimu katibu wa Bunge, John Joel, akisoma
wasifu wa marehemu, alisema Kapteni Komba
aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa
njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es
Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya
shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya
Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia
alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo
lililochukua maisha yake.
Mazishi hayo yalishuhudiwa na viongozi
mbalimbali, akiwamo Edward Lowassa, ambaye
alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na
Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa
Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani
Kikwete, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na
Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Uwanja wa ndege
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, viongozi
mbalimbali waliwasili kwa ndege za kukodi na
Lowassa ndiye aliyefungua mlango kwa ndege
iliyotua saa 2:33 asubuhi akiambatana na
mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani.
Haikupita muda mrefu, ndege nyingine ilitua saa
2:50 ikiwa na Spika Makinda na msafara wake
uliomjumuisha mbunge wa Ludewa, Deo
Filikunjombe.
Saa 3:22 ilitua ndege iliyobeba ujumbe wa CCM
ukiongozwa na Kinana. Wengine waliokuwamo
ni naibu katibu mkuu ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, katibu wa
itikadi na uenezi, Nape Nnauye na mwimbaji wa
kikundi cha TOT, Khadija Kopa. Pia baadaye
Rais Kikwete alitua na ndege ya Serikali.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni