SERBIA ina makocha wa soka zaidi ya 270 na bado wanazidi kuibuka wapya kila kukicha. Moja kati ya sifa za makocha wa nchi hiyo ni ujanja wa kucheza na akili za wachezaji ili kutengeneza matokeo. Wanaujulia mpira wa Kiafrika, wanajua kuigiza hata kuzuga kuendana na mazingira ya sehemu husika ndio maana hawabanduki kirahisi kwenye ardhi ya Afrika. Mfano mdogo Kostadin Papic na Sredejovic Milutin ‘Micho’ ambao waliwahi kuinoa Yanga, ni makocha wenye mbwembwe kuanzia kwa mashabiki mpaka kwa wachezaji na wanajua kuwajaza upepo wachezaji wapambane kiume hata katika mazingira ambayo hayawezekani. Mserbia wa Simba, Goran Kopunovic, naye yupo hivyo na amefanya kituko kimoja katika maandalizi yake ya mechi dhidi ya Yanga ya keshokutwa Jumapili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Unajua amefanya nini? Amefanya jambo ambalo kwa jinsi wachezaji wa Simba wanavyomkubali kwa sasa, hawawezi kukubali litokee. Kocha huyo mwenye mkataba wa miezi sita unaomalizika mwisho wa msimu, Jumanne usiku alizungumza na wachezaji wake mjini hapa na katika moja ya mambo ya kusikitisha aliyowaambia ni pale alipowaaga kwamba endapo watafungwa na Yanga basi huenda akatimuliwa. Mmoja wa wachezaji wa Simba aliidokeza Mwanaspoti kwamba bosi huyo amewaambia kwamba anawatakia kila la heri kama ikitokea bahati mbaya wamepoteza mchezo na yeye akapoteza kazi yake. Mwanaspoti imebaini kwamba wachezaji wametokea kumkubali kocha huyo hivyo gia aliyotumia ni kama kuwahamasisha wachezaji wake wajitume na kuifunga Yanga jambo ambalo lilijionyesha kwenye mazoezi yaliyofanyika juzi Jumatano jioni ambapo wachezaji walionekana kuwa na morali ya hali ya juu. “Kocha katuaga wakati anazungumza na sisi, unajua ana historia ya kufukuzwa kwa Maximo(Marcio), hivyo anaona kama Maximo alifukuzwa Yanga kwa kufungwa na sisi, je ikitokea sisi kupoteza mechi hiyo itakuwaje kwake? Hivyo anaamini pengine na yeye atafukuzwa, tunapambana kuhakikisha Yanga hawatoki na kumlinda kocha wetu,” alisema mchezaji huyo tegemeo wa kikosi cha kwanza. ADVERTISEMENT Goran ambaye amefunga kuzungumza na vyombo vya habari mpaka baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara, huenda aliaga mapema kutokana na historia aliyokutana nayo ya kutimuliwa kwa makocha mara tu wanapofungwa na timu pinzani kama ilivyokuwa kwa Maximo baada ya mechi ya Nani Mtani Jembe alipokubali kichapo cha mabao 2-0. Habari kutoka ndani ya kambi hiyo, zinasema kuwa Goran amekuwa na wasiwasi na matokeo ya mechi hiyo na kulazimika kuwasisitiza wachezaji wake wacheze kwa kujituma ili kumlinda asisitishiwe kibarua chake ingawa Mwanaspoti linajua kwamba uongozi wa Simba una mipango mirefu na Goran. Goran alitua Simba baada ya uongozi kusitisha mkataba wa kocha raia wa Zambia, Patrick Phiri ambaye alishindwa kutimiza malengo kutokana na timu yao kusuasua kwenye ligi, Phiri alifundisha mechi nane na kati ya hizo alishinda moja tu na nyingine zote kutoka sare. Hata hivyo, Phiri alikutana na Yanga mara mbili ambapo mechi ya Ligi Kuu Bara walitoka sare ya bila kufungana huku akishinda mechi ya Mtani Jembe na kufukuzwa baada ya kufungwa na Kagera Sugar bao 1-0. Wakati kocha huyo anarudi kwao Zambia alitoa neno moja kwa Goran kuwa ili ajiwekee imani kubwa kwa wanachama na viongozi wa Simba ni lazima ashinde mechi yao na Yanga ambayo itachezwa keshokutwa Jumapili. Kwa sasa Simba inashika nafasi ya nne kwenye msimammo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 23 wakati Yanga wao wanaongoza wakiwa na pointi 31, jambo ambalo Simba wametamba kuwa watashinda mechi zao zijazo na kuwasimamisha Yanga. MAKOMANDOO SABA Yanga ipo Bagamoyo moja ya sehemu tulivu na ni kawaida kwao kuweka kambi huko, kama Yanga hawajaweka kambi Bagamoyo basi hutimkia Pemba ama watabaki Dar es Salaam lakini pamoja na hayo habari za ndani zinasema wametuma makomandoo wao saba kuichunguza Simba inafanya nini visiwani hapa. Mratibu wa Simba ambaye pia ni mjumbe wa kuteuliwa, Abdul Mshangama ameliambia Mwanaspoti akisema: “Tunawafahamu waliokuja hapa ni akina nani, kikao chao walikifanya jijini Dar es Salaam na kuwatuma watu wao hapa, kuna makomandoo watatu na wazee wao wanne lakini kamwe hawatuwezi.”
GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni