Jumatatu, 23 Machi 2015

MIKATABA YA OWINO,NDEMLA YAFUTWA YANGA,MSUVA STOP.

KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm, ambaye ni miongoni mwa makocha wachache wenye misimamo kwenye Ligi Kuu Bara, ameapa kwamba ndani ya mkataba wake na Yanga, si Said Ndemla, Joseph Owino, Ivo Mapunda, Haroun Chanongo, Amri Kiemba wala Shabaan Kisiga hakuna atakayevaa jezi ya Yanga. Wachezaji hao sita wanamaliza mikataba yao na Simba msimu huu na mpaka sasa hawajaongezewa huku viongozi wa Mnyama wakihofia kwamba Yanga inaweza kuwatia kitanzi muda wowote mastaa wao wawili; Owino na Ndemla. Kocha huyo ambaye viongozi wa Yanga wametokea kumwamini sana amesisitiza kwamba pia hataruhusu kiungo mshambuliaji wao, Simon Msuva kusajiliwa na Wekundu wa Msimbazi. “Msuva namjua vyema kuliko mashabiki wanavyomjua najua umuhimu wake, lakini pia najua mapungufu yake ukiangalia yanazidi kupungua muda unavyozidi kwenda,ni mchezaji anayehitajika hapa Yanga ni vyema sasa mashabiki wakamuacha acheze aisaidie timu, nikiwa hapa Yanga siwezi kufanya kosa la kumuacha aondoke hasa kwenda Simbam,” alisema. “Nimepanga jambo moja nikiwa kocha wa Yanga, sitasajili mchezaji yeyote kutoka Simba hata awe na ubora kama Lionel Messi wa Barcelona, nimegundua jambo moja hata wakija hapa hawaaminiki na watu wa Yanga ni vyema tukasajili kutoka timu zingine lakini sitasajili kutoka Simba.” Kauli hiyo ya kocha huyo amezima ndoto za mastaa hao wa Simba kupewa mikataba na Yanga kwani hata uongozi wa juu umeonywa na wanachama kwamba wasisajili mtu yeyote kutoka Simba kwa vile hawana msaada na wanafanya Yanga inakuwa mteja kwa Simba kila wanavyokutana katika mechi zao. Wanachama matajiri wa Yanga wamekuwa na tabia ya kununua wachezaji mahiri wa Simba kila inapofika mwisho wa msimu ili kudhohofisha wapinzani wao, lakini hali hiyo huenda mwaka huu ikashindikana mpaka mkataba wa Pluijm utakapomalizika mwishoni mwa mwaka ujao na hata ukimalizika huenda akaongezwa kama ufanisi wake ukiimarika. Katika hatua nyingine, Yanga juzi Jumammosi walitumia Sh5 milioni ndani ya saa tatu kuwanunulia viatu maalumu wachezaji kwenye mechi dhidi ya Mgambo JKT iliyopigwa Tanga na Yanga kushinda mabao 2-0. Hiyo ilitokana na Uwanja wa Mkwakwani,Tanga kujaa matope kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku moja kabla ya mechi hiyo. Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano, Mhandisi Isaac Chanji, ambaye aliambatana na mjumbe wake katika kamati hiyo, Yusuphed Mhandeni na Katibu wa timu hiyo Dk. Jonas Tiboroha, mabosi hao walilazimika kutumia kiasi hicho kununua viatu hivyo maalumu ambavyo vilitumiwa na wachezaji kupata ushindi huo muhimu. “Kweli walinunuliwa viatu, isingekuwa rahisi kupambana na viatu vya kawaida katika uwanja kama ule, lakini sio wote waliovitumia kuna wengine walitumia vyao,” alisema Pluijm.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni