Ijumaa, 6 Machi 2015

YANGA YATEGUA MTEGO.

YANGA imesoma alama za nyakati ikaamua kumwondoa kikosini beki, Juma Abdul, ambaye ana kadi tatu za njano. Mabosi wa Jangwani wamesisitiza kwamba wao ni wajanja zaidi ya Simba na kanuni wanazijua hivyo hawatakubali kuingia kwenye mtego wa Mnyama. Katibu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, ameliambia Mwanaspoti jana Alhamisi akisema: “Hatutamtumia Juma Abdul, kanuni tunazijua, hatutaki kuingia kwenye mtego kama wa Simba.” Simba ilimchezesha mchezaji Ibrahimu Ajib mwenye kadi tatu za njano jambo ambalo lilizua utata kwa klabu pinzani ingawa Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) limesisitiza kwamba kanuni zilibadilishwa na ilichofanya Simba si kosa. Katika mazoezi ya jana asubuhi, Mholanzi wa Yanga Hans Pluijm alitengeneza kombinesheni mbili, yoyote inaweza kuanza dhidi ya Simba Jumapili jioni kwenye Uwanja wa Taifa. Baada ya ile ya Simon Msuva, Mrundi Amissi Tambwe na Mrisho Ngassa, sasa ametengeneza nyingine mpya ya ambayo ni Mliberia Kpah Sherman, Jerson Tegete na Hussein Javu. Katika kudhihirisha ubora wake, kombinesheni ya kina Tegete iliwatoa nishai kina Tambwe baada ya kuwachapa mabao 2-1 katika mazoezi yao ya Jumatano yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Uvuvi cha Mbegani Bagamoyo, Pwani. Sherman ambaye alicheza kwa kasi mechi hiyo, alishirikiana vizuri na Javu pamoja na Tegete hadi wakafanikiwa kuibuka na ushindi huo. Katika mchezo huo wa dakika 90 uligawanywa katika vipindi vitatu kila kimoja cha dakika 30. Pluijm na msaidizi wake, Charles Boniface, walikuwa pembeni wamekaa na kurekodi matukio mbalimbali na walipokwenda kwenye mapumziko, kila mmoja walimsomea mapungufu yake ili ajirekebishe. Kubwa alilokuwa anawasisitizia ni kutopoteza nafasi, pasi zenye malengo ziwe fupi au ndefu. Katika mazoezi hayo, Sherman aliondoa gundu baada ya kufunga bao la ushindi.

GAZETI MWANASPOTI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni