SIMBA ipo visiwani hapa ikiendelea na maandalizi yake ya mwisho mwisho ya mchezo wao na Yanga ambao ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara lakini wametoa kali moja tu kwa watani wao kwamba dharau kutapatapa zitawaponza watakapokutana machinjioni pale kwenye Uwanja wa Taifa. Vikao mbalimbali vya kuiangamiza Yanga vilianza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wanachama uliofanyika Jumapili ya wiki iliyopita na Rais Evans Aveva alitamka wazi kuwa ni lazima wawafunge wapinzani wao na kuondoka na pointi tatu muhimu jambo ambalo liliungwa mkono na wanachama wote waliohudhuria mkutano huo. Kikosi hicho kiliwasili Jumatatu visiwani hapa kikiwa chini ya Kocha Goran Kopunovic ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuishuhudia timu yake ikicheza na watani wao mechi inayokuwa na presha kubwa na changamoto nyingi na anatakiwa kuhakikisha hafungwi na ili kujijengea imani na wanachama kwa timu hiyo. Simba inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Amaan na Goran ameamua kuwapa mazoezi wachezaji wake asubuhi na jioni, asubuhi huanza saa tatu na tayari kunakuwa na jua kali na hali ya joto ili kuendana na mazingira ya Dar es Salaam ambako mechi hiyo itachezwa. Mechi hiyo itachezwa Jumapili Uwanja wa Taifa. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Idd Kajuna aliliambia Mwanaspoti kuwa badala ya mazoezi hayo kuanza mapema kabla ya saa tatu, kocha ameamua kubadili ratiba na kusogeza muda mbele na tayari jua linakuwa limekwishakomaa. “Tuna uhakika wa kuifunga Yanga, kikosi chetu ni kizuri kuliko chao, tuna kila sababu ya kuibuka na ushindi, timu ipo katika hali nzuri na hakuna mchezaji ambaye ni majeruhi, kocha amebadilisha muda na sasa wanaanza wakati jua limechomoza na kuna joto, yote haya ni kutokana na hali ya hewa ya Dar es Salaam ambako wachezaji wetu wamezoea,” alisema huku akisisitiza kwamba wanaitaka Yanga machinjioni. Akizungumzia kwa upande wa suala la Ibrahim Ajibu kucheza mechi dhidi ya Prisons akiwa na kadi tatu za njano alisema kuwa: “Yanga wanatapatapa na hiyo inaonyesha ni kiasi gani wanamwogopa Ajibu na atawafunga, sisi tulifuata taratibu zote za kumchezesha mchezaji huyo, hatukukurupuka kumtumia.” Beki Joseph Owino alisema wapo katika morali kubwa ya kupata ushindi kwenye mechi hiyo huku akiwatahadharisha Yanga kuacha dharau kwa kuwa timu yao imefanya vibaya msimu huu na kwamba dharau hizo ndizo zitakazowaponza. “Sisi tunasikia kauli zao, kauli hizo za dharau ndizo zitakazowaponza wafungwe na hivyo ndivyo inavyokuwa siku zote tunapokutana nao unajua kwenye ligi hutakiwi kuidharau timu yoyote kwani kila timu inakuwa imejipanga vizuri, Yanga wajiandae kupokea kipigo, kikubwa tunawaomba mashabiki wetu kutupa sapoti kuanzia sasa na kuendelea,” alisema. Viongozi na wanachama wa Simba wanaendelea na vikao mbalimbali vya ushindi jijini Dar es Salaam na imedaiwa kuwa, vigogo hao wanaweza kuingia visiwani hapa muda wowote kuanzia sasa ili kuwapa motisha wachezaji wao pamoja na kuendelea kuwajenga kisaikolojia kuhusiana na mechi hiyo. PHIRI ATOA SALAMU Kocha Patrick Phiri ambaye alitimuliwa na Simba mwishoni mwa mwaka, ameitakia kila la kheri timu hiyo na kumtaka Goran kupanga kikosi chenye uzoefu na mechi za Simba na Yanga. “Hizo mechi zinakuwa na mambo mengi, yoyote anaweza kushinda ila naamini Simba watafanya vizuri kwa sababu Yanga wanapokutana na Simba wanakuwa na hali ya kujiamini sana jambo ambalo si zuri katika michezo, ukijiamini unaangushwa ndicho kitakachowakumba Yanga. “Pia kocha anatakiwa kuangalia wachezaji wa kuwapanga kwa kuangalia zaidi wenye uzoefu wa mechi za Simba na Yanga, vinginevyo anaweza asifanikiwe jambo ambalo litamweka katika wakati mgumu,” alisema Phiri ambaye msimu huu kabla ya kuondoka amekutana na Yanga mara mbili, mara ya kwanza walitoka sare ya 0-0 katika mechi ya ligi, na kupata ushindi mechi ya Nani Mtani Jembe. Kwa sasa Simba inashika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 23 wakati Yanga wenyewe wapo kileleni wakiwa na pointi 31.
GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni