Jumapili, 1 Machi 2015

WAASI MALI WAKATAA KUSAINI MAKUBALIANO YA AMANI.

Mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati ya serikali ya Mali na makundi ya waasi wa kaskazini wanaotaka kujitenga yamemalizika leo katika mji mkuu wa Algeria, Algiers, lakini muungano wa waasi umekataa kusaini makubaliano ya amani. Awali maafisa wa Algeria walikuwa wamesema makubaliano yamefikiwa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa miezi saba. Vuguvugu linalowania uhuru wa eneo la jamii ya Tuareg, CMA ambalo linaundwa na makundi matatu, limesema linahitaji muda zaidi kuitafakari rasimu ya makubaliano hayo. Mazungumzo hayo yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Algeria yanataka uhuru zaidi wa majimbo ya kaskazini mwa Mali kujiamulia mambo yao, na yanaitaka serikali ya mjini Bamako kutumia asilimia 30 ya mapato yatokanayo na kodi kwa ajili ya maendeleo ya kaskazini mwa nchi. CMA imesema makubaliano hayo hayatekelezeki kwa sababu hayaungwi mkono na umma wa Mali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni