MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amemfungulia kesi kigogo wa Friends of Simba na mmoja wa wafadhili wa muda mrefu wa timu hiyo, Musley Al Ruweh kwa madai ya kumjeruhi mwanawe, Mehbub Ally Manji Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mchezo wa watani hao. Kwa mujibu wa Musley alisema kwamba alipigiwa simu na Polisi wa kituo cha kati, Dar es Salaam akitakiwa kwenda kutoa maelezo ya kumjeruhi mtoto wa Manji. Alipoulizwa chanzo cha matatizo yao, Musley alisema kwamba mtafaruku ulitokea kwenye lifti. “Baada ya mechi mimi nilikwenda kwenye lifti kupanda nishuke chini niende kwenye vyumba vya wachezaji. Nilipofika kwenye lifti watu walikuwa wengi, ikabidi nijichomeke nijibane. “Kwa bahati mbaya lifti ikawa haiendi kwa sababu ilikuwa imejaa. Likatolewa wazo watu wapungue, sasa katika watu waliokuwa mbele mmoja wao alikuwa huyo mtoto wa Manji, mimi simjui. Yule mtoto akashuka mwenyewe. “Aliposhuka, Manji kumbe alikuwa nyuma yangu, akanivaa akaanza kunishambulia kwa maneno kwamba mimi nimemsukuma mwanawe, wakati si kweli. Yule mtoto alishuka mwenyewe. “Kwa kweli mimi sikutaka kupigana naye, na watu wakasema nimuache kwa sababu ana hasira za kufungwa. Alinikunja hadi akanivua kitambulisho changu. Lifti ilipofika chini, mimi nikaenda kwenye chumba cha wachezaji. "Nasikia Manji alikuja hadi kule ananitafuta, lakini sikumfuatilia. Mimi nikaondoka zangu. Sasa nimepigiwa simu naitwa polisi. Nitakwenda kesho (jana). Ila baada ya pale tulifanya jitihada za kuyamaliza haya, lakini Manji alikataa,” alisema Musley.
GAZETI MAJIRA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni