YANGA imeamua kupiga bandika bandua baada ya kuwaamuru wachezaji wote waliokuwa Botswana kikazi kupitiliza moja kwa moja kambini Bagamoyo. Uongozi ulikutana katika kikao kifupi cha kujadili mipango ya kupata ushindi katika mechi zao mbili zijazo na wakakubaliana kwamba kikosi chao kilichorejea jana Jumapili kiende kambini moja kwa moja uamuzi ambao uliwakera wachezaji, lakini hawakuwa na jinsi. Yanga iliitoa BDF XI ya Botswana Ijumaa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kuwachapa jumla ya mabao 3-2 licha ya yenyewe kulala 2-1 katika marudiano, awali ilishinda 2-0. Ikiwa Botswana katika hoteli ya Oasis ilipokuwa imeweka kambi, wachezaji wake waliletewa taarifa ya ratiba hiyo ya kupitiliza kambini na wakashtuka. Mwanaspoti linafahamu kwamba lengo la mabosi wa Yanga ni kutaka kuona wachezaji wao hawapati nafasi ya kukutana na mtu yeyote kuwaharibu kabla ya mechi yao na Simba itakayochezwa Jumapili. Baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ndiyo wataachwa waende makwao. Staa mmoja wa Yanga anayecheza nafasi ya mshambuliaji amealiambia Mwanaspoti kwamba walipanga kuigomea ratiba hiyo, lakini kila walipojaribu kutoa hoja zao zilikubalika kwa baadhi ya viongozi wao wa benchi la ufundi lakini viongozi wakakomaa. “Hawa viongozi wakatili sana, hebu fikiria tangu tumetoka Mbeya hatujapumzika tumekuja huku na wanataka tukitoka huku tena tuingie kambini moja kwa moja tumegoma lakini imeshindikana, unajua wamefanya uamuzi na wakamuachia mzigo katibu aje atuambie ambaye hawezi kubadilisha walichokubaliana na wakubwa wake,” alisisitiza. Akizungumzia hilo Katibu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha alisema wamesikia hoja za wachezaji wao, lakini kwa sasa uamuzi wa kwenda kambini kwenye hoteli ya Kiromo iliyopo Bagamoyo upo palepale hakuna mabadiliko. “Nimeambiwa kwamba walitaka kukataa lakini hilo haliwezekani tunajua umuhimu wa ushindi katika mechi hizi mbili kama unavyojua jinsi mazingira ya mechi yetu na watani yanavyokuwa,” alisema Tibohora. Katika hatua nyingine, BDF ya Botswana wamemuita bosi mmoja wa Yanga kutaka kumsajili mshambuliaji wa Mliberia, Kpah Sherman huku pia wakiteta na kiungo Haruna Niyonzima. Mazungumzo hayo ya BDF wameyafanya na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ambapo mara baada ya mchezo huo wa marudiano kumalizika, bosi wa BDF alimfuata na kuuliza taratibu za kupata huduma za mshambuliaji huyo mwenye nguvu. BDF katika mazungumzo yao walishangazwa na Yanga kumpa dakika chache mshambuliaji huyo ambaye katika dakika zake 11 alizofanikiwa kuingia alionyesha kitu maalum ambacho kiliwavutia. Akithibitisha hilo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro, ameliambia Mwanaspoti kuwa bado hawajaanza mazungumzo rasmi na timu hiyo lakini walichofanya BDF ni kuonyesha utayari wa kuwataka Sherman na Haruna, Naye Haruna alisema: “Wamenifuata baada ya mchezo yule, niliongea na kocha wao, ameniuliza juu ya mkataba wangu nimemwambia bado upo akaniambia kama nataka kuondoka Yanga niwajulishe.” GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni