Ijumaa, 13 Machi 2015

WACHEZAJI SIMBA MARUFUKU.

WACHEZAJI kadhaa wa Simba wakiwamo, Joseph Owino na Said Ndemla, mikataba yao inafikia kikomo. Akilini mwa wachezaji hao ni kwamba endapo Simba ikizingua wanaweza kuibukia Yanga, lakini mambo Jangwani yamebadilika, wazee wamebana. Uongozi wa Yanga umefanya kikao kilichotumia saa nne na viongozi wa matawi na wanachama wao kujadili mwenendo wa timu yao, lakini katika majadiliano hayo mabosi wa klabu hiyo wameambiwa waachane kabisa na kuwasajili wachezaji wanaotoka Simba. Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, amesema katika kikao hicho viongozi hao waliutaka uongozi wao wa juu kuacha kuwapa nafasi wachezaji wanaotoka Simba kwa madai kuwa hawana mchango mkubwa katika timu yao. Sanga alisema wanachama hao wametaka kuangaliwa upya mfumo wa usajili na wametamka kwamba wengi wa wachezaji hao wamekuwa wakishindwa kupambana vya kutosha wanapokutana na Simba. Mmoja wa vigogo wa usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe alitamka baada ya ushindi wa bao 1-0 na Yanga kwamba, vijana hao wa Jangwani hawawezi kupiga hatua kwa vile wanategemea wachezaji wengi wa Simba. “Wametaka tuachane na kuwasajili wachezaji kutoka Simba wanasema wengi wao hawana mchango mkubwa tunapokuwa tunacheza dhidi ya Simba,” alisema Sanga ambaye kitaaluma ni Mhandisi wa Ujenzi. “Tumewasikia mapendekezo yao, lakini uongozi tutafikiria ni nini cha kufanya kama mchezaji mzuri na yupo katika timu hiyo tunafanyaje?” “Labda tunaweza tukamsajili halafu tusimchezeshe tunapocheza dhidi ya Simba ili kuondoa matatizo. “Lakini hayo ni mawazo na bado hatujafikia uamuzi wa mwisho juu ya hili.” Imani hiyo imetokana na Yanga kuonekana kuzidiwa na Simba katika mechi za hivi karibuni.

GAZETI MWANASPOTI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni