WAKATI Simba wakiweweseka na kasi ya mabao aliyonayo Simon Msuva wa Yanga, kinara huyo wa mabao wa Ligi Kuu ni kama amewafichulia siri yake. Msuva mwenye mabao 11, matano kati ya hayo akiyafunga kwa kichwa, mawili kwa penalti na manne kwa mguu alifichua kuwa wala si uchawi kama watu wanavyofikiria bali ni ujanja wake wa kuiba muda wa kocha wake, Mholanzi Hans Pluijm wanapokuwa mazoezi ili kujifunza kufunga ndiyo sababu ya kumfunika Didier Kavumbagu mwenye mabao 10. Aliweka wazi kuwa, amekuwa akiwasumbua, Juma Abdul na Mnyarwanda Mbuyu Twite mara kwa mara wampigie mipira ya krosi na yeye amalizie kufunga kwa kichwa au mguu huku makipa, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’ akiwaomba wakae golini. Alisema, amekuwa akifanya hivyo karibu kila kipindi cha mazoezi na kila mmoja amekuwa anamwomba ampigie mipira mitano au sita na kwa upande wa makipa mbali na kuokoa mipira hiyo ya krosi, huwa anawapigia mipira mingine mitano ya penalti kila mmoja. Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema: “Ninatamani kufunga, napenda nifunge na hamu yangu ni kufunga lakini pale ninapoweza faida ya klabu na mimi mwenyewe, nikawa nafanya sana mazoezi ili nifanikiwe.” “Nimekuwa nikiwasumbua sana baadhi ya wachezaji mazoezini, huwa naibia mwalimu anapokuwa amesimamisha programu yake kwa muda mfupi, huwa nawaomba wanipigie krosi na mimi nijaribu kufunga kwa kichwa na miguu makipa wakiwa golini. Wakati mwingine nawaomba pia wachezaji wa katikati wanichezeshee mipira nayo nafunga ni hivyo tu,” alisema Msuva ambaye amefunga mabao ya kichwa katika mechi waliyocheza na Prisons mzunguko wa kwanza bao moja, raundi ya pili mawili dhidi ya Prisons, moja na Mbeya City na moja dhidi ya Azam. “Lakini pamoja na hamu yangu hiyo, huwa silazimishi kufanya hivyo, ninapokuwa sina uwezo, pia namwomba Mungu anilinde na majeraha ili nitimize malengo yangu ya kufunga kadri niwezavyo ili niwe mfungaji bora na timu yangu ichukue ubingwa.” Msuva ambaye kuna habari kwamba Simba inamuwania pia aling’ara kwa mabao kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambalo hata hivyo ni mahasimu wao Simba ndio waliobeba taji la michuano hiyo.
REKODI
Awali Msuva alikuwa anacheza straika wa kati katika klabu mbalimbali alizopitia kama, Azam FC, Moro United na timu za Taifa za vijana chini ya miaka 17 na 20. Baada ya kutua Yanga, alihamishiwa pembeni nafasi ya winga na yeye anasema: “Sina tatizo kucheza nafasi hiyo, kama una uwezo wa kufunga mabao, kokote utafunga iwe straika wa kati au winga pembeni.” Kocha wake mkuu, Mholanzi Hans Pluijm amesifu kiwango cha Msuva kuwa ni mchezaji anayefuata maelekezo na kukubalia mabadiliko. Umahiri wa Msuva unakaribiana na ule waliokuwa nao wachezaji Mrisho Ngassa na Mussa Hassan Mgosi ambao ni mawinga, lakini walioweza kunyakua tuzo ya Ufungaji Bora katika Ligi ya misimu ya nyuma kwa kufunga mabao 16 kila mmoja katika msimu wake. Kasi hiyo ya Msuva kwa mechi saba zilizosalia kwa timu yake kabla ya kufunga msimu inaweza kumfanya amfikie aliyekuwa Mfungaji Bora msimu uliopita Amissi Tambwe aliyefunga mabao 19. Hata hivyo, uwiano wake wa mabao unampa wakati mgumu kufikia rekodi hiyo ya Tambwe aliyemzidi mabao mawili Kipre Tchetche aliyekuwa kinara wa mabao msimu wa 2012-2013.
GUMZO MWANZA
Wakati nyota wa Yanga wakitua jijini hapa kwa ajili kambi ya Taifa Stars inayojiandaa kucheza na Malawi kesho Jumapili, Msuva amekuwa gumzo midomoni mwa mashabiki wa soka wa Mwanza baada ya kutoonekana kwenye mazoezi na wenzake. Mashabiki wameingiwa na mchecheto na kuhoji alipo Msuva na kudai kama hatakuwemo ni wazi Malawi itakuwa na kazi rahisi kushinda. Wachezaji wa Yanga walionekana kambi ya Stars ni Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mrisho Ngassa waliotua juzi Alhamisi, walipasha kidogo uwanjani kabla ya kuondoka na gari la Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba na Kocha wa Toto Africans, John Tegete. “Tumefurahi kuwaona nyota wa Yanga wakijumuika na Stars, lakini hatujaridhika na tuna mashaka makubwa kwani hatujamuona Msuva na muda wa mazoezi ni mdogo sijui kama wataweza kuwahimili wa Malawi,” alisema Selemani Mashimba. Hakuna kiongozi wala kocha aliyekuwa tayari kuzungumza jambo lolote la timu hiyo kwa madai watazungumza siku moja kabla ya mchezo. Katika mazoezi ya juzi ya mashabiki iliongezeka na kama Chama cha Soka Mwanza (MZFA) wangeamua kuwatoza kiingilio cha Sh1000 basi wangepata pesa za maana. Mashabiki wengi walikuja ili kuwaona nyota hao wa Yanga tofauti na hali ilivyokuwa katika mazoezi yaliyopita. Hata hivyo, wakati mashabiki wakiwa na hamu na Msuva, strika Mbwana Samatta aligeuka kivutio kikubwa kwenye upigaji wa penalti katika mazoezi hayo ya juzi baada ya kumtungua Mwadini Ally kwa mikwaju saba jambo lililomfanya kipa huyo abaki akicheka tu.
GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni