KOCHA wa Simba, Goran Kopunovic, juzi Alhamisi jioni alitumia muda kama wa dakika tano kuzungumza na mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi, baada ya wachezaji wote kuondoka uwanjani wakiwa wamemaliza mazoezi yao. Mazoezi hayo yalifanyika Uwanja wa Amaan hapa Unghuja, Zanzibar huku kila mchezaji akionekana kuwa katika morali kubwa ya pambano lao la kesho Jumapili dhidi ya watani wao Yanga ambao wameweka kambi yao mjini Bagamoyo. Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itachezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Goran alionekana akimpa maelekezo mshambuliaji huyo raia wa Uganda jinsi ya kutumia uwanja hasa katika upatikanaji wa mabao ama utengenezaji wa mabao kwa wenzake, huku Okwi akimtoa wasiwasi kocha huyo. Goran hakutaka kuweka wazi zaidi mbinu za kuwaua wapinzani wake hao ambao kwake ni mara ya kwanza kukutana nao ingawa alisema wachezaji wake wote wapo vizuri na anaamini watashinda mechi hiyo. “Naandaa timu si kwa mechi moja, nataka tufanye vizuri zaidi ya hapa, nimesikia upinzani uliopo kati ya hizi timu ndiyo maana nakiandaa kwa ushindi wa mechi zote, katika mchezo huo nataka wachezaji wangu wacheze kwa kasi na kushambulia zaidi. Najua Yanga ni nzuri lakini mimi huwa najiandaa na huwa sihofii ukubwa wa mechi ninachotaka ni ushindi,” alisema. “Nimekaa na wachezaji wangu kwa muda mwingi, nimezungumza nao juu ya hiyo mechi na ukubwa wake, nimewajenga kisaikolojia, nataka ushindi wa mechi hii na nyingine zijazo.” Mazoezi hayo mazito yalikuwa ni ya mwisho kwa timu hiyo ambayo inatarajia kurudi Dar leo Jumamosi ambapo jana Ijumaa asubuhi aliamua kuwapumzisha wachezaji wake huku jioni wakienda kufanya mazoezi ya kunyoosha mwili tayari kwa kuivaa Yanga inayoongoza kwenye ligi ikiwa na pointi 31, Simba ina pointi 23 na inashika nafasi ya nne. Kocha Goran aliwafundisha wachezaji wake jinsi ya kumiliki mipira na kupiga mipira ya juu wakiwa katika eneo la nje ya 18 ambapo Isihaka, Joseph Owino, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda na Said Ndemla ndiyo walifanikiwa kupiga mashuti yaliyogonga mwamba kama kocha alivyowataka wafanye huku wengine wakishindwa. Vigogo wa Simba walitarajia kuwasili visiwani hapa baadaye jana ili kuwahamasisha wachezaji wao ikiwamo kuwapa ahadi ya fedha endapo wataifunga Yanga. Pia walitarajiwa kuongoza dua kwa wachezaji wao ili waweze kuifunga Yanga hapo kesho katika mechi hiyo ya mzunguko wa pili wa ligi inayosubiriwa kwa hamu.
GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni