Jumatatu, 2 Machi 2015
SIMBA WAIONYESHA YANGA BAO TATU.
Simba waionyesha Yanga bao tatu
RAIS wa Simba, Evans Aveva, alipokuwa anawania kuingia madarakani alionyesha ishara ya vidole vitatu juu akimaanisha kwamba pointi tatu kila mechi, lakini aliteleza kidogo ila sasa amekuja kivingine kwa kudai kuwa pointi tatu zilianza juzi Jumamosi walipoifunga Prisons mabao 5-0. Pia akasisitiza hakuna bifu baina ya viongozi wa Simba bali ni majungu tu ya watu.
Kali zaidi ametamka kuwa makali yao wanayahamishia kwenye mechi ya watani wao Yanga wanaoongoza Ligi Kuu Bara kwa kuwa na pointi 31. Timu hizo zitavaana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku jana Jumapili aliamua kuiondoa timu yake jijini na kuipeleka Unguja, Zanzibar kama ilivyo kawaida yao wanapokutana na watani wao.
Hata hivyo viongozi hao walidai kushtukia mbinu za chinichini ndani ya TFF kutaka kusogeza mbele mechi dhidi ya Yanga wikiendi ijayo.
Simba ina imani kubwa kwamba ikiwa visiwani humo mara nyingi hupata matokeo mazuri na kwa vile wamedhamiria kwa nia moja huku wakiungana na wanachama wao kuiangamiza Yanga, wameona ni vyema kikosi chao kukiondoa mapema Dar es Salaam.
Simba imetua Zanzibar jana mchana na Yanga ikijichimbia Bagamoyo baada ya kutua kutoka Botswana. Katika mkutano wa wanachama wa Simba uliofanyika jana Jumapili kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay na kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 400 ulikuwa na ajenda tatu, Aveva alifafanua sababu za timu hiyo kufanya vibaya katika msimu huu wa ligi ingawa sasa Simba inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 23.
Mkutano huo uliopangwa kuanza saa 3:00 asubuhi ulianza saa 5:00 kwani wanachama waliohudhuria mkutano huo walifika kwa kusuasua huku wakionekana hawana maandalizi na mkutano huo. Hata hivyo Aveva alitumia saa 1:30 kumaliza mkutano huo.
“Ni lazima tuwafunge Yanga, napenda kusema kwamba pointi tatu ndiyo zimeanza sasa, hata kwa Yanga lazima tuchukuwe pointi tatu na itawezekana,” alisema Aveva huku Kamati ya mashindano kupitia Makamu Mwenyekiti Idd Kajuna ikiongeza:
“Tumesikia tetesi kuwa TFF (shirikisho la soka) wanataka kusogeza mechi yetu na Yanga, sasa tunatoa kama angalizo kuwa wasijaribu kufanya mabadiliko yao ya ratiba tunataka mechi ichezwe kama ratiba inavyoonyesha na muda uliopangwa.”
Mkutano huo ulikuwa na ajenda tatu, Mradi wa Bunju, Wanachama wapya na kadi mpya za wanachama ambazo hazikujadiliwa ila zilisomwa kama taarifa tu wakati ajenda ya mwenendo wa timu ndiyo iliyopewa nafasi ya kujadiliwa.
Rais huyo aliwaambia wanachama wake kuwa klabu yao inakabiliwa na ukata mkubwa na hivyo kusababisha mambo mengine kukwama.
“Hatuna vyanzo vingi vya fedha, tunategemea wadhamini, wanachama na viingilio katika mechi ambavyo pia vimeshuka na tumepeleka malalamiko kuhusu tiketi za elektroniki,” alisema.
GAZETI MWANASPOTI.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni