KOCHA wa Simba, Goran Kopunovic, amesema wachezaji wapya watatu walichangia kuimaliza Yanga juzi Jumapili. Akizungumza na Mwanaspoti, Kopunovic raia wa Serbia yenye makocha zaidi ya 270 wa soka la kulipwa, alisema alilazimika kutumia mfumo ambao hawakuwahi kuutumia lengo likiwa kuwabana Yanga akiwatumia wachezaji wake watatu vijana ambao beki Kessy Ramadhan, kiungo Abdi Banda na kiungo Ibrahim Ajibu huku kila mmoja akipewa jukumu lake. Kopunovic alisema alijua Yanga nguvu yao kubwa ni katika mashambulizi ya pembeni ambapo alimtaka Kessy kuwa imara katika upande wa kulia akishirikiana na Tshabalala huku Wekundu hao wakitumia upande wa kulia kuanzisha mashambulizi mpango ambao ulijibu kwa kupatikana kwa bao hilo pekee katika kipindi cha pili likifungwa na Emmanuel Okwi. Alisema mbali na mpango huo, pia alimpa jukumu Banda ambaye alicheza mechi yake ya kwanza ya Simba na Yanga akitakiwa kuzima mipango yote ya Yanga kutoka kati kwa kurudi haraka kusaidia ukabaji wakati Yanga wakishambulia mpango ambao ulifanikiwa huku Ajibu akipewa jukumu la kusaidiana na Okwi. “Nawajua Yanga naweza kusema kwamba niliwasoma kule Zanzibar wakati tukishiriki ile michuano (Kombe la Mapinduzi) nikajua nitakapokutana nao nifanye nini ndiyo maana sikuwaangalia tena baada ya hapo nilimaliza kazi lakini kuna watu ambao niliwatuma kumaliza mechi,”alisema Kopunovic. “Unapokutana na timu yenye wachezaji wazoefu kama Yanga ni lazima utumie akili ya ziada, niliwapa majukumu wachezaji wapya kazi ya kuizima Yanga ambao walishirikiana na wenzao kukamilisha ushindi.”
GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni