Jumanne, 3 Machi 2015

WANAJESHI WA CONGO WAWAUA WAASI WA FDLR.

Jeshi la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo limewauwa waasi saba kuwakamata wengine kadhaa, kuzidhibiti ngome zao na kukamata silaha katika kampeini ya kutokomeza uasi mashariki mwa Congo inayoingia siku ya saba hii leo. Msemaji wa serikali ya Congo Lembert Mende amesema mwanajeshi mmoja ameuawa tangu kunazishwa kwa operesheni ya kijeshi wiki iliyopita kupambana na waasi wa kundi la Democratic Forces for the Libertaion of Rwanda FDLR katika majimbo ya Kivu Kaskazini na kusini. Mende amesema waasi hao kutoka Rwanda wanaandamwa na jeshi na wanakimbia na kuacha nyuma nyingi ya silaha zao na kuongeza sio kitisho kikubwa kama walivyokuwa wakiishi katika ngome zao. Kundi hilo la waasi wa FDLR linakisiwa kuwa na kati ya wapiganaji 1,500 hadi 2,000 wakiwemo wanajeshi wa zamani wa Rwanda na waasi waliohusika katika mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994. FDLR imesababisha maafa makubwa Congo Waasi hao wamepora madini yaliyo mashariki mwa Congo yakiwemo dhahabu, almasi na bati na wameendeleza vita dhidi ya serikali ya Congo na makundi mengine ya waasi tangu kutorokea Congo baada ya mauaji ya halaiki Rwanda na wanatuhumiwa kwa kuhusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za bindamu nchini Congo ikiwemo mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watoto vitani. Wachambuzi hata hivyo wanasema waasi hao wa FDLR wanalifahamu vizuri eneo hilo la mashariki mwa Congo na watakimbilia maeneo ya vijijini badala ya kusubiri kupata hasara ya kupoteza wapiganaji wake na silaha katika mapambano kati yao na wanajeshi. Zaidi ya waasi 50 waliokamatwa na wanajeshi walionyeshwa kwa vyombo vya habari hapo jana katika mji mkuu wa jimbo la Kivu ya kaskazini wa Goma. Kwa jumla waasi 93 wamekamatwa katika majimbo mawili ya Kivu ksakazini na Kusini tangu wiki iliyopita. MONUSCO haishirikiani na Congo Baada ya opresheni dhidi ya FDLR kucheleweshwa kwa majuma kadhaa Congo ilianzisha kampeini ya kijeshi Jumanne wiki iliyopita hata baada ya Umoja wa mataifa kutangaza rasmi kuwa haitashirikiana na jeshi hilo la Congo katika operesheni ya kuwatokomeza waasi wa FDLR kwasababu ya kukataa kwa serikali ya Congo kuwaachisha kazi majenarali wawili wa jeshi wanaoutuhumiwa na umoja wa Mataifa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Mende amesema kujiondoa kwa jeshi la Umoja wa Mataifa MONUSCO kutoka operesheni hiyo imewarejesha nyuma hatua kidogo lakini akasisisitiza hawana uhasama na MONUSCO na watadhihirisha kuwa nchi hiyo ina uwezo wa kujilinda. Mende ametangaza pia kuwa jeshi limetanua operesheni hiyo hadi kaskazini mwa jimbo la Katanga linalopakana na Zambia na Angola. Mapambano makali yameripotiwa pia katika mbuga ya wanyama pori ya Virunga ambako waasi hao wamejificha. Jeshi la Congo limeapa kuendelea na operesheni hiyo ya kuwasaka waasi wa FDLR hadi watakapokubali kuijsalimisha au kurejeshwa nchini mwao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni