Jumatatu, 23 Machi 2015

SIMBA KUTEMA MIZIGO.

KLABU ya Simba ipo mbioni kuwatema wachezaji ambao wameonekana mzigo ndani ya klabu hiyo katika msimu huu. Habari za ndani zimewataja wachezaji hao ni pamoja na Simon Sserunkuma aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili wa klabu hiyo mwishoni mwa mwaka jana. Wengine ni walioshindwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza karibu msimu mzima na kuoneakana wana kula mshahara na posho bure. “Kamati ya Usajili ilikutana mwishoni mwa wiki na kuwajadili wachezaji hao mizigo na wameamua mwishoni mwa msimu waachwe hasa wale waliomaliza mikataba yao na wenye mikataba mirefu watasitishwa,” kilisema chanzo chetu. Kiliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha msimu ujao Simba inaunda kikosi imara kwa kusajili wachezaji watakaokuwa msaada kwa timu yao tofauti na sasa wakisuasua na kutokuwa na hakika ya kurejesha taji la Ligi Kuu linaloshikiliwa na Azam na linalowaniwa pia na watani za Yanga. Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspoppe, alikanusha kuwepo kwa mipango hiyo, licha ya kukiri kukutana kuwajadili wachezaji wao. “Hatukukutana ili kujadili wachezaji wa kuwaacha, tulikutana kuwajadili wachezaji waliomaliza mikataba yao kwa lengo la kuona tunafanya nini kwa ajili ya msimu ujao,” alisema Hanspope na kuongeza kwamba uamuzi uliofikiwa katika kikao hicho ni kuwaongezea mikataba mipya wachezaji hao ingawa Mwanaspoti linajua kwamba wengi watatemwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni