Mnyama aliye hatarini kutoweka ulimwenguni Leo ni siku ya wanyama na mazao ya porini duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon ametaka umakini zaidi katika kushughulikia vitendo vya uhalifu dhidi ya maliasili hiyo. Katika ujumbe wake, Ban amesema biashara haramu ya wanyamapori na bidhaa zitokanazo na viumbe hivyo ikiwemo ndovu, magogo na kifaru, imekuwa ikiibuka na mbinu mpya kila uchao na hata kuzidi ile ya usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya. Amesema kushamiri huko kunapigiwa chepuo na rushwa na uongozi dhaifu akiongeza kuwa kuna ushahidi thabiti wa kuhusika kwa mitandao ya kihalifu iliyopangwa na vikundi vilivyojihami. Ban amesema biashara hiyo haramu siyo tu inakwamisha utawala wa sheria bali pia unatishia usalama wa taifa na ni kikwazo kikubwa kwa juhudi za wanavijiji na jamii za watu wa asili za matumizi endelevu za maliasili. Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka umakini wa kushughulikia uhalifu huo akitaka ushiriki wa jamii zote zinazohusika na matumizi ya maliasili hizo kwa ajili ya dawa, chakula, ujenzi, samani, urembo na nguo. Amesema endapo usimamizi wa sheria utakwenda sambamba na ushirikishi wa jamii nzima kutawezesha kumaliza tatizo la matumizi haramu ya bidhaa za porini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni