VIONGOZI wa Simba, wamegundua kwamba walibugi kumpiga chini straika wao namba moja wa msimu uliopita, Amissi Tambwe ambaye sasa anatamba na kuwapa kiburi Yanga kutokana na uwezo wake wa kutupia kwenye nyavu. Vigogo hao wameingia msituni kumsaka mchezaji huyo kwa udi na uvumba ili arudi Msimbazi haswa baada ya Kocha Mserbia, Goran Kopunovic kuwaambia mabosi wake kwamba mchezaji huyo bado ni kifaa na anamhitaji. Lakini Yanga wamemuweka chini Tambwe na kumwambia atulie watampa maisha bora na kitendo cha timu hiyo kushiriki michuano ya kimataifa ndicho kimempagawisha zaidi aendelee kubaki Jangwani ambapo amemhakikishia Kocha Hans Pluijm kwamba harudi Simba hata kwa dawa. Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm ambaye ni Mholanzi, amesema amezungumza na Tambwe juu ya maisha yake ya baadaye ambapo raia huyo wa Burundi amemhakikishia kwamba hawezi kurudi Simba msimu ujao. Pluijm alisema Tambwe ambaye mpaka sasa ameshaifungia Yanga mabao saba katika mashindano ya aina mbili bado ni mchezaji muhimu katika kikosi chake baada ya kukubalika katika mfumo wa timu hiyo. “Nimesikia hizo taarifa kwamba kuna watu wanataka kumrudisha Simba, nikazungumza na Tambwe na amenihakikishia kwamba hawezi kukubali kurudi huko tena kwani anafuraha akiwa hapa na timu yetu, jambo zuri ni kwamba Tambwe ni mchezaji wetu anayefanya vizuri nafurahia anavyojituma katika timu ameweza kufanya kile ambacho makocha tunamtaka afanye uwanjani, katika hilo unawezaje kumruhusu mtu kama huyo aondoke katika timu yako?” alisisitiza Pluijm. Hata ushiriki wa Yanga kwenye michuano ya kimataifa umemfanya mchezaji huyo kutuliza akili Yanga kwa madai kwamba mbali na kushiriki msimu huu kwenye Kombe la Shirikisho hata mwakani kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki tena huku nafasi ya Simba ikiwa finyu kutokana na kuchechemea kwenye ligi ya ndani. “Sijajua kwa nini Tambwe aliachwa, anafanya vizuri tunahitaji mtu kama huyo katika timu yetu, ukiangalia kwa sasa tuna mtu mmoja tunayemtegemea katika ufungaji Okwi, anakosa msaidizi, namjua vyema Danny (Sserunkuma ) lakini ameshindwa kufanya vizuri,”alisema Kopunovic. “Nilikuwa mshambuliaji, namjua mshambuliaji mzuri, angalia Chelsea walikuwa na shida ya ufungaji wakamsajili Diego Costa sasa anafunga, siku zote mchezaji mzuri ni yule anayefanya vizuri katika wakati husika,”alisisitiza kocha huyo ambaye kuna uwezekano mkubwa akamtema Sserunkuma ambaye tayari ameshaomba kupunguza urefu wa mkataba wake aondoke Simba baada ya mambo kutomwendea vizuri.
GAZETI MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni